HABARI MPYA

6/recent/ticker-posts

MAKALA: Jeshi la Polisi Mkoani Njombe Laimarisha Ulinzi Shirikishi na Mapambano Dhidi ya Ukatili Wa Kijinsia

Polisi Kata ya Mlangali, Mkaguzi wa Polisi INSP Lilian Marcel, akiwa na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ulayasi iliyopo Wilaya ya Ludewa, Mkoani Njombe alipotembelea shule hiyo kutoa elimu.

Na mwandishi wetu- NJOMBE

KATIKA kuimarisha amani, usalama, na usitawi wa jamii, Jeshi la Polisi mkoani Njombe kupitia Polisi kata limeendelea na ziara mbalimbali za utoaji wa elimu kwa wananchi na wanafunzi.

 

Hatua hii inalenga kujenga uelewa kuhusu ulinzi shirikishi, ukuzaji wa uchumi halali, na utokomezaji wa ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto katika wilaya mbalimbali za mkoa huo.

 

Katika kutekeleza mkakati huo, Polisi Kata ya Makambako, Mkaguzi wa Polisi INSP Maria Mwise, alikutana na kufanya mazungumzo na wananchi wa Mtaa wa Jogoo uliopo Wilaya ya Kipolisi Makambako.

 

Katika mkutano huo wa ushirikishwaji jamii, INSP Mwise aliwahimiza wananchi Kujishughulisha na biashara halali Ili kujipatia kipato kisichokuwa na shaka na kuepuka migogoro ya kisheria.

 

Alieleza, “kujihusisha na biashara haramu kunahatarisha usalama na kuingiza jamii kwenye matatizo ya kisheria hivyo. wananchi mnatakiwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za kuaminika kuhusu viashiria vya uhalifu ili hatua zichukuliwe kwa wakati kabla ya kuleta madhara.” 

Polisi kata ya Ulembwe Wilaya ya Wanging'ombe,Mkaguzi wa Polisi INSP Manyerere Kiwuyo, akitoa elimu ya kisheria na ulinzi shirikishi kwa wananchi wa kata hiyo.

Nae Polisi Kata ya Mlangali, Mkaguzi wa Polisi INSP Lilian Marcel, akitoa elimu kwa wanafunzi wa Shule ya Sekondari Ulayasi iliyopo Wilaya ya Ludewa, aliwataka wanafunzi kujiepusha na mazingira hatarishi yanayoweza kupelekea kufanyiwa vitendo vya ukatili.

 

Pia INSP Lilian aliwataka wanafunzi kutoogopa kutoa taarifa mapema kwa Jeshi la Polisi, walimu, au wazazi mara wanapoona viashiria vya ukatili ili hatua za kisheria zichukuliwe mara moja.

 

“Mnapoona kuna viashiria vya mtu kutaka kuwafanyia ukatili, msiogopoe kutoa taarifa, waambieni walimu, wazazi wenu au njooni kwetu Jeshi la Polisi tuna kitengo maalum cha dawati la jinsia na kazi yetu ni kushughulikia kesi hizo. Msisubiri mpaka vitendo vitokee kwani vinasababisha madhara makubwa kwako na jamii kwa ujumla,” alieleza mkaguzi huyo.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto INSP Eliminata Amani akizungumza na mwanafunzi Shule ya Sekondari Itambo wakati akitoa elimu katika shule hiyo. 

Katika Wilaya ya Wanging'ombe, Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto INSP Eliminata Amani akifuatana na Polisi Kata ya Mdandu INSP Happy Japhet, walitembelea Shule ya Sekondari Itambo.


Habari zinazohusiana: MADEREVA WALIOFUNGA TAA KALI KWENYE BAJAJI WANASWA NJOMBE 

 

Ziara hii ya utoaji elimu ililenga kukabiliana na ukatili wa kijinsia na ukatili dhidi ya watoto, ambapo wakaguzi hao walisisitizaWanafunzi kusoma kwa bidii na kudumisha nidhamu ili kujiepusha na mazingira yanayohatarisha usitawi wao.

Polisi Kata ya Uwemba INSP Teddy Kossam akitoa elimu kwa wananchi.

 Katika kuhakikisha ulinzi Shirikishi na Kufichua Wahalifu Polisi Kata ya Uwemba INSP Teddy Kossam aliwahimiza wananchi kuimarisha ushirikiano na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za siri mapema zitakazosaidia kufichua na kuzuia vitendo vya uhalifu kabla havijatokea.


"Usalama wa mtaa au kijiji unategemea zaidi mchango wa wananchi wenyewe wanaolinda maeneo yao na kuwafichua wahalifu wanaoishi miongoni mwao."
INSP Teddy Kossam

 

Nini kifanyike Kama Jamii?

Jitihada hizi za Jeshi la Polisi Mkoani Njombe zinadhihirisha kuwa ulinzi na usalama unaanzia kwa mwananchi mmoja mmoja.

 

Kutoa taarifa za usahihi, kulinda watoto dhidi ya ukatili, na kujishughulisha na shughuli halali za kiuchumi ndiyo nguzo kuu ya jamii salama na yenye maendeleo.

 

Hivyo, wananchi wanasisitizwa kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za kuaminika kuhusu viashiria vya uhalifu ili kulinda amani na usalama katika jamii na taifa

Post a Comment

0 Comments