Wananchi mkoani Njombe wametakiwa kuungana kupaza sauti na kukataa kwa pamoja vitendo vya ukatili wa kijinsia katika maeneo yao ili kuwezesha jamii kuendelea kuwa sehemu salama kwa makundi yote hasa wanawake na watoto.
Rai hiyo imetolewa na mkuu wa operesheni na mafunzo mkoa wa Njombe, Kamishna msaidizi wa Polisi (ACP) Abubakary Kunga akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi mkoa huo wakati wa ufunguzi wa maadhimisho ya Kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa kijinsia iliyofanyika wilayani Wanging'ombe.
Amesema kila mmoja anao wajibu wa kulinda ustawi na haki za wengine hasa watoto katika jamii badala ya kusubiri wafanyiwe vitendo vya ukatili jambo ambalo linapelekea madhara zaidi kwao na taifa kwa ujumla.
Aidha amewataka kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria mapema kwani kuendelea kuwanyamanzia bila kuchukuliwa hatua kunawapa nguvu wahalifu kuendelea kuumiza wengine zaidi.
Kwa upande wake mkuu wa Dawati la Jinsia na ulinzi wa mtoto mkoa huo, mrakibu msaidizi wa Polisi (ASP) Oscar Kitaly amesema dhumuni ya maadhimisho ya kampeni hiyo ni kuunganisha nguvu za wadau katika kujenga jamii isiyovumilia ukatili wa kijinsia na kulinda usalama na haki za kila mtu.
Kwa upande wake Katibu Tawala Wilaya hiyo Veronica Sanga, amesema vitendo vya ukatili wa kijinsia vinaathiri maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla, hivyo ili kuwezesha kuwa na jamii yenye maendeleo bora ni lazima kila mmoja kuchukia vitendo hivyo kwa vitendo.
Nae afisa maendeleo, Halimashauri ya Wilaya Njombe, Herieth Magaji, amehimiza jamii kujenga utaratibu wa kuandika mirathi ili kuepuka kuacha migogoro ya kifamilia pale mmoja wa mwanafamilia anapofariki dunia.
Kampeni ya Siku 16 za Kupinga ukatili wa Kijinsia huadhimishwa kila mwaka kuanzia novemba 25 hadi disemba 10 ambapo kwa mwaka huu inabebwa na kaulimniu isemayo, "Tuungane kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto; Jenga Taifa imara lenye haki na usawa kuelekea dira 2050."




0 Comments