HABARI MPYA

6/recent/ticker-posts

VIKUNDI VYA UJASIRIAMALI VINAVYOWAIMARISHA WANAWAKE KUWA VIONGOZI


 Na Essau Kalukubila.

Kwa miongo kadhaa kumekuwa na tafsiri kinzani kuhusu dhana ya uongozi Visiwani Zanzibar jambo ambalo limepelekea kuwakosesha fursa ya msingi wanawake kushiriki katika nafasi za uongozi kutokana na tafsiri potofu kuhusu ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

Nini maana ya uongozi?

Uongozi ni uwezo wa kuweza kuyakabili kwanza maisha yako binafsi ambapo wengine husema ni uwezo wa kuyatawala maisha yako kulingana na taratibu ambao wewe mwenyewe  umejiwekea  kuanzia ndani ya familia  yako  ukifanikiwa  hili unakuwa umefaulu  katika mtihani  huu wa kwanza  wa uongozi  ndipo  jamii  inapoanza  kukuona kuwa hata ukawaongoza wao pia. 

Sehemu kubwa ya jamii yetu hapa Zanzibar imekuwa ikimwangalia mwanamke kwa dhana tofauti na kumhusisha ama kudiriki kumtolea hukumu huku akionekana kama kiumbe kisichoweza kuleta maendeleo katika jamii.

Pamoja na hilo, lakini katika miaka ya karibuni tumeshuhudia namna wanawake kadhaa ambao walipata fursa ya kuongoza kwa ustadi na weledi mkubwa kuliko hata wanaume pamoja na kukabiliwa na changamoto kadhaa.

Katika hili ni dhahiri kwamba mwanamke akipatiwa fursa na kujengewa mazingira ya kuondoa vikwazo vinavyochangia kumfanya ashindwe kufikia kuwa kiongozi, anaweza kuwa kiongozi mzuri katika nafasi aliyopata.

Mkoa wa Kaskazini Pemba ni miongoni mwa mikoa ambayo imeonekana kutoa kipaumbele kikubwa kwa wanawake katika nafasi mbalimbali kuanzia ngazi za chini na wanawake hao wamekuwa wakifanya vizuri na hata kuwazidi wanaume.

 Aisha Hussen Abdalla ni kaimu mwenyekiti wa baraza la Mji Wete alisema ushiriki wa wanawake katika nafasi mbalimbali ndani ya mkoa huo umesadia kuongeza usawa wa maamuzi katika mambo mbalimbali jambo ambalo awali lilikuwa halipo.

“Kutokana na kuwepo kwa ushirikishwaji wa wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi kwenye jamii, imefika muda ambapo yale maamuzi yanayotolewa na vyombo mbalimbali vinazingatia usawa wa kimawazo ya kila upande,” alisema.

Aidha alibainisha kuwa changamoto kubwa ambayo bado inatatiza ufikiaji wa usawa katika nafasi za uongozi ni kuwepo kwa baadhi ya wanaume ambao hawajakubali katika uwezo wa wanawake kuwa viongozi jambo ambalo wakati mweingine linapelekea kuangalia madhaifu ya baadhi ya wanawake kuwaona kama wanawake hawawezi.

“Unajua wanaume wengi wanapenda sana kutumia mifano ya baadhi ya wanawake ambao pengine kwa madhaifu yao walishidwa kutekeleza majukumu yao lakini wanasahau kwamba wanawake nao ni binadamu, ila wanatumia mwanya huo kuwaponda wanawake utafikiri wanaume wao hawakosei,” alisema. 

Katika vikundi vya ujasiriamali, ushiriki wa wanawake pia umeongezeka kutokana na jinsi wanawake wanavyoshiriki kuwa sehemu ya uongozi kupitia vikundi hivyo.

Bikombo Faki mwanakikundi cha Umoja ni Nguvu Shehia ya Makangale Wilaya ya Micheweni, alisema mwamko wa wanawake kushirki katika uongozi umeongezeka kuanzia katika vikundi kwani wanawake wameanza kuwa viongozi katika vikundi hivyo.

Alisema, “wanawake tunashukuru tumeanza kuamka kujiingiza katika nafasi za uongozi kwani kwasasa ukija katika vikundi vyetu viongozi wengi ni wanawake kuliko wanaume. 

Nae Shadia Ame alisema kutokana na ushiriki wa wanawake kushika nafasi za uongozi katika vikundi hivyo inawasaidia kuwajengea ujasiri wa kukua katika masuala ya uongozi.

“Kwakweli huku kwenye vikundi wanawake wengi wameanza kupata mwamko na ujasiri wa kuzidi kugombania nafasi za uongozi kwani kupitia humu wanawake wengi wanapata kufahamu namna ya kuongoza n ahata ikitokea fursa nyingine nje yah apo inakuwa ni rahisi kugombea nafasi huyo,” alisema Shadia.

Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania, TAMWA Zanzibar, imekuwa  ikifanya kazi kubwa  ya kuielimisha jamii  kuachana na mawazo mgando ya  kuwa mwanamke  hawezi kuongoza.

Fat-hiya Mussa Said, mratibu wa TAMWA ofisi ya Pemba alisema chama hicho kipo katika utekelezaji wa mradi wa Ushirikishaji wanawake katika uongozi unaolenga kuhamasisha wanawake kugombea nafasi hzizo.

Alisema, “mradi wetu wa ushirikishaji wanawake katika uongozi unaofadhiliwa na Ubalozi wa Norway unalenga zaidi kuwahamasisha wanawake kuwa na uwezo wa  kudai haki zao za kuwa viongozi katika nafasi mbalimbali kuanzia ngazi za chini.”

Ni wazi kwamba ushiriki wa wanawake katika uongozi huongeza uwiano sawa wa kimawazo katika maamuzi yanayofanywa kuhusu jambo husika, na ili kuweza kufikia lengo hili ni lazima jamii ibadili mtazamo na kumuona mwanamke katika jicho la uongozi na si vinginevyo.

Post a Comment

0 Comments