![]() |
Kampeni ya "Tuwaambie Kabla Hawajaharibikiwa" imewafikia rasmi wanafunzi wa Shule ya Sekondari Njombe Technical School ikiwa na lengo la kutoa elimu dhidi ya vitendo vya ukatili.
Elimu hiyo imetolewa na Polisi Kata ya Mlangali Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe, Mkaguzi wa Polisi, INSP Lilian Marcel wakati alipofika shuleni hapo kuzungumza na wanafunzi hao ambapo ameeleza kuwa lengo kuu la kampeni hii ni kuwajengea uwezo watoto pamoja na jamii kwa ujumla ili kutambua kwa urahisi viashiria vya ukatili.
Kupitia elimu hiyo, wanafunzi wanafundishwa mbinu mbalimbali za kujilinda dhidi ya udhalilishaji, unyanyasaji na aina zote za ukatili ambazo zinaweza kuhatarisha maisha na mstakabali wa masomo yao.
INSP Lilian ameeleza kuwa kampeni hiyo imeweka mkazo mkubwa katika kuwafundisha wanafunzi hao njia sahihi na salama za kuripoti taarifa za ukatili wa kijinsia.
Wanafunzi wamehamasishwa kutokaa kimya pindi wanapokumbana au kushuhudia vitendo hivyo, badala yake watoe taarifa haraka kwenye madawati ya jinsia, au kwa walimu na wazazi wanaowaamini.
Aidha amesisitiza kuwa kinga ni bora kuliko tiba, na ndiyo maana Jeshi la Polisi limeamua kuwafuata wanafunzi shuleni ili kuwapa elimu kabla madhara hayajatokea na uelewa huo utawasaidia wanafunzi kuwa mabalozi wema wa kupinga ukatili shuleni na katika jamii zinazowazunguka.
![]() |


0 Comments