Na mwandishi wetu NJOMBE
Katika kuadhimisha Miaka 20 ya Polisi Jamii, Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe, limetumia fursa hiyo kwa kuungana na wananchi kufanya mazoezi ya pamoja kupitia POLISI NJOMBE JOGGING ikiwa na lengo la kuonesha umuhimu wa mashirikiano katika kukuza na kulinda amani na mshikamano baina ya jeshi na wananchi.
Mazoezi hayo ambayo yameongozwa na Mkuu wa Polisi Jamii mkoa huo, Kamishna msaidizi wa Polisi ACP Assel Mwampamba yamewakutanisha wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya mji wa Njombe.
Akizungumza baada ya kushiriki mazoezi hayo ACP Mwampamba ameeleza kuwa jeshi la Polisi kwa miaka 20 limekuwa likitekeleza dhana ya Polisi jamii ambayo lengo lake kuu ni kuwaunganisha pamoja wananchi na jeshi hilo ili kushirikiana katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu kwenye maeneo yao.
Amebainisha kuwa kupitia michezo na mazoezi hayo, wananchi wanapata fursa ya kuwa karibu zaidi na askari jambo ambalo linasaidia kukuza mahusianao chanya baina yao.
Aidha amewataka wananchi mkoani humo kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi hasa Polisi kata waliopo kwenye maeneo yao kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa wakati kabla hawajasababisha madhara kwao na jamii kwa ujumla.
Katika hatua nyingine amewasisitiza wananchi kuendelea kujitokeza kwa wingi katika mazoezi hayo ya pamoja kupitia POLISI NJOMBE JOGGING ambayo hufanyika kila siku za jumamosi kwani licha ya kuwa yanasaidia kukuza mahusiano na jeshi hilo lakini pia ni sehemu ya kuimarisha afya kwa kujikinga na maradhi yasiyoambukiza.
Maadhimisho ya miaka 20 ya Polisi Jamii nchini yanaendelea chini ya kaulimbiu inayohimiza ushirikiano kati ya jamii na Jeshi la Polisi katika kudumisha amani, usalama na umoja wa kitaifa.
Kupitia maadhimisho hayo, elimu kwa wananchi inaendelea kusisitizwa kuwa ni nyenzo muhimu katika kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu ikiwa ni pamoja na kujenga jamii iliyo salama.
0 Comments