TAMWA ZNZ , Kitengo cha habari
Chama cha
waandishi wa habari Wanawake Tanzania, TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na wadau wa
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwemo Taasisi ya kukabiliana na mabadiliko
ya tabianchi (ZACCA) na Afisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais Zanzibar, imeandaa
mkutano wa kwanza wa mabadiliko ya tabianchi utakaofanyika Zanzibar, oktoba 20 hadi 22 katika Ukumbi wa
Idrissa Abdulwakil.
Akizungumza
na waandishi wa habari katika ofisi za TAMWA Tunguu, Mkoa wa Kusini Unguja,
Mwenyekiti wa kamati ya Jukwaa la mabadiliko ya tabianchi Zanzibar.(ZANCCC)
Mahfudh Shaban Haji, amesema lengo la mkutano huo ni kujenga uwezo, uelewa na
hamasa kwa asasi za kiraia, wanajamii na Idara za Serikali kufahamu dhana nzima
ya mabadilikoya tabianchi na uhimili wake.
Aidha Shaaban ameeleza kuwa mkutano huo
utazungumzia mada mbali mbali za kimataifa na kitaifa ikiwemo mkakati wa
mabadiliko ya tabianchi wa mwaka 2014, sera, uwajibikaji na dira ya maendeleo
2050 ambayo inakwenda sambamba na mipango ya kimataifa ya maendeleo endelevu ya
SDGs.
‘’Mabadiliko
ya Tabianchi ni suala mtambuka hivyo tutajenga uelewa juu ya mchango wa asasi
za kiraia, kuimarisha usimamizi na utekelezaji wa uhifadhi na uhimili wa
mabadiliko ya tabianchi,” Mahfoudh.
Nae Mkurugenzi
wa Chama cha Waandishi wahabari Wanawake Tanzania, TAMWA ZNZ Dkt Mzuri Issa
amewataka waandishi wa habari kuandika habari zinazoibua changamoto za
mabadiliko ya tabianchi ili ziweze kuwafikia walengwa na kufanyiwa kazi.
‘’waandishi wahabari tumieni kalamu zenu
kuyaibua na kuyafanyia uchechemuzi masuala ya mabadiliko ya tabianchi kwa upana
wake’’ Dkt Mzuri Issa TAMWA ZNZ.
Kwa upande
wake mwakilishi wa Taasisi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ZACCA
Ngwali O. Ngwali amesema Ukataji wa mikoko unachochea zaidi Mabadiliko ya tabia
nchi katika maeneo ya fukwe za bahari ambapo katika maeneo ya
Mkokotoni,fungurefu na Donge kwa Mkoa wa Kaskazini Unguja, yameathirika kwa
kiasi kikubwa.
Aidha
amewaomba wanajamii kuyalinda mazingira ili kuirithisha Zanzibar ya kijani kwa
lengo la kuepuka athari zinazoendelea kujitokeza.
Jumla ya
washiriki 250 kutoka ndani na nje ya Zanzibar watashiriki mkutano huo,
unaotarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Afisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,
Mh Harusi Said Suleiman na kauli mbiu ni “ imarisha uhimili wa mabadiliko ya
tabianchi Zanzibar “
Mwisho
0 Comments