| Hawra Shamte,mtafiti |
| Mratibu wa miradi ya kupinga udhalilishaji TAMWA ZNZ, Zaina Salum akizungumza. |
SERIKALI imeshauriwa kukarabati na kuboresha
miundombinu ya Mahakama maalum ya udhalilishaji Zanzibar ikiwa ni pamoja na kuwezesha
matumizi ya ushahidi wa kielektroniki hasa kwa kesi zinazohusu watoto ili kuwa rafiki
kwa wanaotumia mahakama hizo na kuwezesha upatikanaji wa haki katika mazingira
bora.
Wito huo umetolewa na wadau wa kupinga udhalilishaji Zanzibar
wakati wa mkutano wa kuwasilisha ripoti ya ufanisi wa Mahkama Maalum katika
kushughulikia kesi za Udhalilishaji tangu kuanzishwa kwake ulioandaliwa na
TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Foundation For Civil
Society (FCS) na Ubalozi wa Norway uliolenga kujadili mstakabali wa watoto
kulindwa dhidi ya vitendo hivyo.
Kwa mjibu wa ripoti hiyo, imeelezwa kuwa licha ya mahakama
hiyo kuonesha mafanikio makubwa ya usikilizaji wa kesi tangu kuanzishwa kwake lakini
bado miundombinu haitoshi kutokana na kukosekana kwa vyombo vya kisasa vya
usikilizaji wa kesi, ikiwemo mifumo ya kidigitali (video conference) na ukosefu
wa vyumba maalum vya kuwaweka watoto walioathirika na vitendo hivyo.
Hawra Shamte, ambaye ni mtafiti wa utafiti huo uliofanywa
na TAMWA ZNZ kati ya Juni 16 na Julai 16, 2023 kwa kuzihusisha Shehia 57 Unguja na Pemba
alisema, “ukosefu wa vifaa katika mahakama na miundombinu duni bado ni
changamoto, mfano majengo ya Mahakama ya Vuga, Mahonda, Mkoani na Wete Pemba ni
ya zamani na karibu kupitwa na wakati wakati jambo linalopelekea ugumu katika
uendeshaji wa kesi hizo.”
Aidha alieleza utafiti umebaini
miongoni mwa mafanikio ya uwepo wa mahakama hiyo ni pamoja na kuongeza kasi ya
usikilizwaji wa kesi za Udhalilishaji katika mahakama hizo.
"Wahojiwa walisema mahakama hii maalum ya Udhalilishaji
inaonesha siku hizi kesi za aina hii zinachukuliwa kwa uzito mkubwa na hata
hukumu zinazotolewa si ndogo kama ilivyokuwa awali, siku hizi utasikia mtu
anapewa kutoka kifungo cha miaka 20 hadi miaka 30 na pia wapo waliopewa
kifungo cha maisha," alieleza Hawra.
Kutokana utafiti kubaini miongoni
mwa changamoto zinazozuia ufanisi wa mahakama hizo ni kesi nyingi
zinazowahusisha vijana wenye umri wa kuanzia miaka 14 hadi 18, waathiriwa kushindwa
kutoa ushirikiano katika kutoa ushahidi, utafiti umeshauri serikali kuongeza
vifaa vya upelelezi ili kuwezesha uchunguzi kukamilika mapema kuepukana na
mashahidi vigeugeu.
“Tunapendekeza serikali kutoa vifaa
vya kutosha kwa idara ya polisi ili kuwawezesha ufanisi katika kufanya
uchunguzi bila kuchelewa ikiwa ni pamoja na kuanzisha na kuwezesha matumizi ya
ushahidi wa kielektroniki kwenye kesi hizi,” alisisitiza mtafiti huyo.
Mratibu wa miradi ya kupinga udhalilishaji TAMWA ZNZ, Zaina
Salum, alieleza TAMWA ZNZ katika kuendelea na kampeni ya kupaza sauti ya Haki
za Watoto dhidi ya matukio ya ukatili kinafanya tafiti mbalimbali ili kukuza
uchechemzi wenye kuchochea mabadiliko chanya kwenye masuala hayo.
Zaina alieleza, “TAMWA ZNZ tumekuwa tukifanya uchechemzi wa
masuala mbalimbali yanayohusu vitendo vya udhalilishaji kupitia tafiti na
kuzifikisha kwa taasisi na wadau husika kuzifanyia kazi ili kuisaidia jamii
kuondokana na tatizo hili.”
Mapema mwenyekiti wa TAMWA ZNZ, Asha Abdi, alishauri jamii kuwapa
nafasi watoto kuchangamana na watoto wenzao kupitia majukwaa mbalimbali ili
kuwajengea uwezo wa uthubutu na ujasiri wa kuzungumza changamoto na fursa
zinazowakabili na kuwalinda dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.
Alisema iwapo watoto watapewa fursa sawa na wazazi kushiriki
kamilifu katika majukwaa yao ikiwemo mabaraza ya watoto kuanzia ngazi ya shehia
itawajenga kukua katika misingi ya ujasiri na kukuza uwezo wa kukabiliana na
vikwazo mbalimbali vinavyo kandamiza haki zao.
Alitaja watoto wa kike wanakosa haki zao ikiwemo haki ya
uongozi kutokana na kukosa misingi ya kushirikishwa katika majukwaa yao kuanzia ngazi ya awali yanayowajenga kutambua
fursa na haki zao muhimu.
“Wazazi tuwaruhusu watoto wetu hasa wa kike wachangamane na
watoto wenzao kupitia mabaraza ya watoto ili wapate fursa ya kuzungumzia mambo
yao yanayowahusu na hii itawasaidia kuwajengea ujasiri wa kuzungumza kwa uwazi
changamoto zao,” alieleza mwenyekiti huyo.
| Wilfred Ezra, afisa uchunguzi kutoka Tume ya Haki za Binaadam na Utawala Bora |
Wilfred Ezra, ambaye ni afisa uchunguzi kutoka Tume ya Haki
za Binaadam na Utawala Bora alishauri jamii kuendelea kutoa taarifa za matukio
ya udhalilishaji yanapotokea ili kusadidia kuwalinda watoto na kuwadhibiti
watekelezaji wa vitendo hivyo.
Nae Thuwaiba Ali, mmoja wa wanafunzi walioshiriki mkutano huo
aliomba serikali kuongeza adhabu kali kwa watekelezaji wa vitendo vya ukatili
ili adhabu hizo ziwe onyo na tishio kwa wenye tabia hizo zinazokiuka haki za
binaadam.
"Serikali iweke adhabu kali kwa wanaofanya vitendo vya
udhalilishaji ili kuwatisha wengine kuendelea kufanya vitendo hivyo kasababu
wengi wanaendelea kutufanyia udhalilishaji kutokana wanajua hata wakifungwa
wataachiwa kwasababu hakuna adhabu kali," alieleza mwanafunzi huyo.
Ayoub Nassor Sharif kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka
alipongeza TAMWA ZNZ kwa kuendelea kuwaunganisha wadau kupaza sauti dhidi ya vitendo
vya udhalilishaji na kushauri kuendelea kutoa elimu kwa jamii kutambua umuhimu
wa kuwenda kutoa ushahidi mahakamani ili watuhumiwa wachukuliwe hatua kisheria.
Aliomba, “TAMWA iendelee kuhamasisha jamii kuja kutoa
ushahidi mahakamani pale wanapohitajika kwani ni kweli kesi nyingi zinafutwa
kutokana na kukosa ushahidi na kama ambavyo tunafahamu hakuna kesi bila
ushahidi.”
Mkutano huo ambao umeandaliwa na TAMWA ZNZ kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wakiwemo Foundation For Civil Society (FCS) na Ubalozi wa Norway umewashirikisha wadau kutoka taasisi mbalimbali za serikali na kiraia wakiwemo mahakimu, waendesha mashtaka, viongozi wa dini, walimu, wanamtandao wa kupinga udhalilishaji na maafisa ustawi wa jamii ambapo nimwendelezo wa maadhimisho ya siku ya mtoto wa kike.
0 Comments