HABARI MPYA

6/recent/ticker-posts

TAMWA yampiga msasa waziri wa fedha bunge la vijana



Na Thuwaiba Habibu.

Elimu ina umuhimu mkubwa katika maisha ya binaadamu, maendeleo ya jamii na nchi kwa ujumla.

Hii ndio iliopelekea kuwemo methali, mafumbo, nukuu na maelezo ya kila aina juu ya umuhimu wa elimu

Miongoni mwao ni Elimu ni ufunguo wa maisha, Elimu ndio hati ya uhakika ya kuwa na safari yenye manufaa, Kutafuta elimu ni kuwekeza kwa maisha mazuri ya baadaye na Mizizi ya elimu ni michungu, lakini mavuno yake yana ladha tamu.

Wapo  wanaosema elimu ni kama mwanga wa kumtoa mtu kwenye kiza na kuweza kuona wapi ndio panapofaa kwenda kwa salama, Amani na furaha.

Hii imethibitika kwa ushuhuda wa uamuzi wa Chama Cha Waandishi Habari Wanawake Tanzania (TAMWA Zanzibar) kushajiisha wanawake kugombea nafasi za uongozi ili kujiendeleza wao na jamii.

Mmoja wa watu walionufaika na mafunzo haya na kuhesabikika kama mmoja wa viongozi bora waliopata haya mafunzo ni Zainab Salehe Salim, maarufu kwa jina la Zasasa.

Zainab ambaye ni mwanafunzi  wa Chuo kikuu Cha Zanzibar (Zanzibar University) alipatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wanawake    kushika hatamu za uongozi.

Dada huyu aliyewahi kuwa Makamo wa Rais katika serikali ya wanafunzi ya chuo alifanya mengi ya mafanikio, ikiwa pamoja na kuwashajiisha wanawake wenzake kushiriki katika michezo na michezo mizuri yenye uhusiano na mila na utamaduni wa Zanzibar,  kama nage na mbio za magunia

Katika safari yake ya uongozi alikumbana na changamoto nyingi, zikiwemo zile ambazo hakuzitarajia ndani na nje ya chuo.

Hata hivyo, hakukata tamaa na  alikataa nia yake ya kuwa kiongozi  kurejeshwa nyuma na badala yake alizichukua kauli za kumkatisha tamaa kama mambo yaliyompa nguvu zaidi za kusonga mbele katika safari yake.

"Iliifika wakati sikutaka  kuendelea kuwa Makamo wa Rais wa serikali ya wanafunzi chuoni. Lakini baada ya kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyokusanya tasisi nyinyi, zikiwemo TAMWA na Chama cha Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) nilipata uelewa mzuri kuhusu uongozi na kuamua kusonga mbele", alisema.

Baada ya kushiriki katika mjadala TAMWA walimchukua na kumpataia mafunzo ya kuwawezesha wanawake katika uongozi na hio kumshajiisha zaidi kubadili maamuzi na kuendelea na uongozi.

Alisema mafunzo yalimuongezea ujasiri na kujuwa vizuri changamoto ambazo mwanawake anatakiwa kuishi nazo anapokuwa kiongozi na kufahammu vizuri njia sahihi ya kupita ili kufanikiwa.

Alivutiwa na elimu iliyotolewa na mmoja wa wanazuoni maarufu wa elimu ya dini ya Kislamu, Profesa Issa Haji Zidi, hasa alipofafanua kwa undani kwamba  dini ya Kiislamu haijakataza mwanamke kuwa kiongozi wala kuwawekea vikwazo.

Kinahotakiwa ni ujasiri na kutokiuka misingi ya dini na maelekezo yaliwekwa na dini ya Kiislamu katika maisha ya mwanamke.

Profesa Zidi alieleza kwa undani kwamba katika enzi ya Mtume Muhammad (SAW) walikuwepo wanawake waliokuwa viongozi katika vita na mambo mengine na kote huko yalipatikana mafanikio chini ya uongozi wao.

Alitoa mfano wa  Bi Nasiba  binti Kaabu  kuwa ni   mmoja wa walinzi majasiri wa Mtume (SAW)  katika vita vya Uhud na kuhakikisha mtume anakuwa salama na alijeruhiwa  takribani mara 11.

Vita vya uhud vilikuwa ni kisasi dhidi ya Waislamu kufuatia  vita vya Badri. Baadhi ya watu mashuhuri wa Quraishi kama vile Abu Jahl, Utbah, Shaiba, Walild, Umayya bin Khalaf, na Hanzala bin Abu Sufyan, waliuawa kwenye vita vya Badr.

Baada ya kifo cha Abu Jahl, uongozi wa watu wa Makka ulipitia kwa mwenza wake, Abu Sufyan, ambaye alikuwa mkuu wa ukoo wa Banu Umayya.

Kitabu kitukufu cha Quran kimethibitisha kuwa mwanamke ana haki sawa na mwanaume na miongoni mwa maelezo yasiyo na mshaka juu ya suala hili yamo katika sura mbali mbali, kama Aya  ya 97 ya Suratul An Nahil.

Maelezo ya surah hii inasema: ‘’Na wakifanya vitendo vizuri wakiwa wanaume au wanawake  basi hao wataingia peponi hawatadhulumiwa hata ugamba wa kokwa ya tende."

Yote hayo ni makatazo yanyoonyesha kuwa hakuumbwa mwanaume kuwa mfalme na mwanamke kuwa mtumishi wa mfalme huyo. Haya ndio yaliyomfanya Bi Zainab kuona kuwa ana uwezo wa kugombea nafasi kubwa zaidi ya uongozi.

 Baada ya kumaliza mafunzo ya TAMWA pakatokea nafasi  katika Bunge la Vijana  la Tanzania ambapo palitakiwa ndani ya kila chuo kikuu  kutoka wanafunzi wawili wenye uwezo na kuzingatiw jinsia. Bila ya kusita aligombea nafasi ya Spika, lakini hakufankiwa.

Matokeo ya kuibuka mshindi wa pili hayakumkatisha tamaa na alifarajika alipochaguliwa kuwa Waziri wa Fedha wa Bunge hilo, nafasi ambayo anaishikilia hadi sasa.

Alisema  nafasi hio aliipata baada ya kuwashawishi viongozi  wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, akiweno Naibu Spika, kumpenekeza  kuwa Waziri wa Fedha wa hilo Bunge la Vijana Tanzania .

 Zainabu ni mpambanaji mzuri anayesaidia wanawake wenzake kuingia katika uongozi kwa lengo la kutaka kufikia asilimia 50 kwa 50 ya wanawake na wanaume katika uongozi.

Anafanya hivi katika harakati za ndani ya chama chake cha CCM na katika shughuli zake za uongozi wa chuoni.

Alisema katika CCM aliweza kumshajihisha Husna Bakari Hamisi kugombea nafasi ya katibu wa  jimbo katika jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), lakini hakubahatika kuibuka mshindi.

Pia alichaguliwa  jaji wa chuo kikuu Cha Zanzibar na Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi ndani ya chuo hicho na kuthibitisha kuwa wanawake   wanaweza kuongoza.

Mratibu  wa kuinua wanawake katika uongozi kutoka TAMWA, Mariyam Ame, alisema hadi sasa waliopatiwa mafunzo ya moja kwa moja  ni 170 (Unguja 100 na Pemba 70) na  wanatarajiwa kuwaelimisha wengine ndani ya vyama  vyao.

 Alisema  kupitia mafunzo hayo wanawake wengi wataweza kujitokeza kugombea nafasi za uongozi ili kweza kufanya kazi sambamba na wenzao wanaume.

Mafunzo hayo  pia  yalijumuisha wanafunzi wa vyuo  vikuu ambapo waliweza kugombea nafasi  ya Serikali ya wanafunzi na Bunge la vijana Tanzania.

Alisema lengo la kutoa mafunzo ni kuitaka jamii kujua haki za kila mtu kugombea uongozi na kufanya juhudi za kuyarekebisha mapungufu ya  sera na sharia yanayomkwaza mwanamke kushika nafasi ya uongozi.

Mjumbe wa Bunge la Vijana Tanzania  ambaye alikuwa Makamo wa Raisi wa Chuo kikuu Cha (SUZA), Arafa Yahya Hamis, amemueleza Zainab kuwa kijana  mwenye sifa nyingi nzuri zilizowafanya wampendekeze kuwa kiongozi.

Mongoni mwa siafa hizo ni mtu asiye na dharau na ambaye anawashauri wenzake njia mzuri za kupita katika kugombea uongozi.

Arafa alisema ni Zainab ni mcheshi na mwenye kupenda mashirikiano katika kufanya kazi.

Rikizi Abdallah Ali ambaye ni miongoni mwa wanawake  waliopata mafunzo ya uongozi yanayotolewa na TAMWA alisema  mafunzo yamemuongezea  uimara katika uongozi wake.

Alipopatiwa mafunzo tayari alishagombea nafasi ya Katibu wa , Itikadi na Uenezi katika CCM katika  Jimbo la Kijito Upele  na nafasi ya Spika wa Bla la Chuo Kikuu Cha Zanzibar (zu).

"Mafunzo yaniongezea kujiamini  na kuniwezesha kuelewa majukumu yangu ni yapi kama mwanamke kiongozi ‘’, aliongeza.

Alisema anaaminiani nafasi za uongozi katika chama sio za wazee tu na kuahidi mnamo mwaka 2025 atajitokeza kugombea uongozi.

Alisema  anayatumia mafunzo aliyoyapata kuhamasisha wanawake kugombea uongozi ili kuonesha wanaweze kuongoza kwa uadilifu na kueleza kuwa mfani mzuri wa uwezo wa mwanamke kuongoza  ni ule wa Mama Samia Suluhu Hassana kama Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Nae Rais wa Serikali ya wanafunzi Wa Zanzibar University,Said Abdallah Hamis, alisema uongozi wa Zainab ni wa kipekee kwa sababu ni wenye hamasa kubwa  kwa sababu anataka kila mtu kupatiwa haki yake .

Alisema wanafunzi wanamuangalia Zainab kama kioo kwa vile hana woga na alifanikiwa kuwapatia wanafunzi  wanaokaa bweni kuwekewa  mazingira rafiki na yanayohakikisha usalama wao.

‘’Zainabu ndio mfano sahihi wa kuiga kwani wakitokea watu kama yeye ambao wanapenda maendeleo basi tutafika mbali katika kuhakikisha wanawake wanashiriki katika nafasi za uongozi’’, aliongeza.

 

 

 

 

 

 


Post a Comment

0 Comments