HABARI MPYA

6/recent/ticker-posts

VIONGOZI WANAWAKE WATARAJIWA WA VYAMA VYA SIASA VYA ZANZIBAR WAPIKWA KIUNGOZI NA TAMWA.

 


Na Riziki Abdalla. 

CHAMA cha Waandishi wa habari wanawake Zanzibar(TAMWA) kimetoa mafunzo maalumu  ya uongozi kuanzia tarehe 20,21 na 22 kwa upande wa Unguja ndani ya mwezi huu wa Machi 2023 kwa wagombea wanawake watarajiwa kutoka vyama mbalimbali vya siasa vya Zanzibar.

Mafunzo hayo yamejumuisha vyama nane 08 vya siasa  vilivyopo unguja  ikiwemo chama cha CCM, ACT Wazalendo, CHADEMA , CUF, ADC, ADA TADEA, UMD,UDP pamoja na viongozi mbalimbali wa Vyuo Vikuu kwa lengo la kuwajengea uwezo wanawake hao kiuongozi wakati wa uchaguzi, ikiwa ni miongoni mwa utekelezaji wa majukumu na malengo ya mradi wa SWILL(Strengthen Women In Leadership) wa kuinua wanawake katika uongozi.

Akifungua mafunzo hayo Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi Wa Habari Wanawake Zanzibar (TAMWA) Dkt Mzuri Issa amewataka viongozi hao kuwa na ujasiri, uthubutu na utayari katika kugombea nafasi za uongozi kwenye nyadhifa yeyote ile  ili kuleta maendeleo bora kwenye shehia, majimbo na hata mikoa. “Kama wanawake tuna haki zote za  kugombea nafasi yeyote ya uongozi ili kuleta maendelea chanya katika nchi yetu” alisema Dkt Mzuri Issa.

Nae Maryam Ame Chum mratibu wa mradi wa kuinua wanawake katika uongozi ameeleza lengo la mafunzo hayo ya uongozi kwa wagombea wanawake watarajiwa  kuwa “  jumla ya wanawake 80 tumekusudia kuwapa mafunzo ya uongozi kati ya hao 45 kutoka Unguja na 35 kutoka Pemba kwa lengo la kuwajengea uimara kwenye harakati za kiuongozi”

Miongoni wa wakufunzi walioweza kuhudhuria na kutoa mafunzo kwa waombea wanawake watarajiwa ni Lutfia Faida Haji ambae ni Afisa jinsia katika kitengo cha Jinsia na Mjumuisho wa Jamii kutoka tume ya uchaguzi Zanzibar kwa lengo la kutoa utaratibu na mwongozo kwa wagombea watarajiwa katika zoezi la kujaza fomu za kugombea wakati wa uchaguzi  kwa utaratibu unaotakiwa. “kwa mujibu wa sharia za Tume Ya Uchaguzi Ya Zanzibar hakuna pingamizi yeyote kwa mwanamke kuingia katika kinyanganyiro cha uongozi ikiwa atatimiza sifa za kugombea na kuchaguliwa” alisema Afisa Jinsia na Mjumuisho wa Jamii. Pia aliongeza kwa kusema “kifungu cha 35 katika sheria ya uchaguzi ya Zanzibar kimetoa fursa kwa wanawake kuwa baraza la wawaikilishi linafikisha asilimia 40 ya nasafi za uongozi kwa wanawake”

Pia Mwanaidi Suleiman Ali ambae ni Afisa wa Uhusiano ZAECA aliweza kuwapa elimu wanawake hao juu rushwa ya ngono na kuwaeleza juu ya jitihada za mapambano zidi ya rushwa Zanzibar ambapo sheria ya kuzuia rushwa ilitungwa mwaka 1975 na mwaka 2012 ilipitishwa na Baraza La Wawakilishi Zanzibar. “kuna aina nyingi za rushwa lakini rushwa hii ya ngono imepewa nafasi kubwa na ndio ndio mbaya zaidi, hivyo mkiwa mnaelekea kwenye uchaguzi wa vyama vyenu ni lazima mkubali kubadiika na kukataa kudhalilika ili kulinda hadhi yako ya ujanajike” alisema Afisa Uhusiano ZAECA.

BAADHI YA WANUFAIKA WA MAFUNZO WAELEZA FAIDA WALIZOPATA KATIKA MAFUNZO HAYO.

Naima Salum Hamadi kutoka chama cha UDP alieleza kuwa “katika uchaguzi wa 2020 niligombea nafasi ya Spika wa Baraza la Wawakilishi kupitia tiketi ya  chama changu cha UDP lakini sikubahatika kushinda ila kupitia mafunzo haya niliyoyapata yamenijengea uwezo hata 2025 nije kugombea tena panapo uhai na uzima.”

Pia Khayam Mustafa Yakuti kutoka Chama Cha Mapinduzi(CCM) alieleza kuwa “ kwa sasa nina nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) katika  jimbo la Malindi na nashkuru kupatiwa mafuzo haya ya uongozi kutoka TAMWA kwani yameniongezea hamasa na kunifanya nijione kuwa natosha kugombea nafasi yeyote ile ya uongozi iwe ya serikali au ndani ya chama”

Nae Yusra Khalid Kombo kutoka chama cha ACT Wazalendo alieleza kuwa “ mimi niliwahi kugombea nafasi ya Udiwani katika wadi ya Mwanyanya jimbo la Mtoni mwaka 2020 kwa kuamini ninaweza na kupitia mafunzo haya yameniongeza ari zaidi ya kuja kugombea tena kwenye uchaguzi wa 2025”

Pia Hudhaimat Kheri Salim ambae ni Makamu Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyuo Vikuu na taasisi za elimu ya juu Zanzibar (ZAHILFE) alieleza kuwa “kwa niaba ya viongozi wenzangu wa vyuoni tutahakikisha mafunzo haya ya uongozi tuliopatiwa na TAMWA tunayetendea haki katika nafasi zetu za uongozi na pia tutakuwa mabalozi wazuri kwa wanafunzi wengine”

Kwa kumalizia, nae mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo ya uongozi Dkt Salim Suleiman Ali aliwasisitiza viongozi hao kujuwa haki zao uongozi katika mchakato wa demokrasia pamoja na kutumia teknolojia ya habari itakayoweza kuwasaidia wanawake katika siasa na kutimiza malengo yao ya uongozi.

Post a Comment

0 Comments