Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman, amesema kuna haja ya kujipanga upya katika kujenga Utalii ili kwenda sambamba na mwelekeo wa Uchumi wa Dunia kupitia maendeleo ya Sekta hiyo Ulimwenguni.
Mhe. Othman ameyasema hayo leo, huko Hoteli ya Park Hayyat Mjini Zanzibar, akihutubia katika Ufunguzi wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani, yanayoadhimishwa Kimataifa, ifikapo Tarehe 27 Septemba ya kila mwaka.
Amesema kuwa hatua hiyo itasaidia kuijenga upya na kuikuza Sekta ya Utalii Nchini, ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya Uchumi wa Zanzibar, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na Mataifa mengine mengi, kote Ulimwenguni.
Mheshimiwa Othman ametaja mambo ambayo yanaweza kusaidia tafakuri katika Sekta hiyo kuwa ni pamoja na Historia na Turathi za Zanzibar; Uimarishaji wa Huduma kwa Watalii wanaowasili Nchini; Kujenga dhana ya Utalii Jumuishi; Kuitambulisha Nchi na Mfumo wake wa Uendeshaji wa Serikali; na Kutangaza Utalii kupitia mbadala wa Vivutio vya utalii viliopo Nchini.
Akitilia mkazo juu ya mbadala huo, Mheshimiwa Othman ameeleza kwa kusema, “kwa muda mrefu sasa, Zanzibar imekuwa ikitangaza au kutegemea zaidi utalii wa mahoteli, bahari na fukwe, na hivyo kuacha kutumia bidhaa nyingi za kitalii zilizopo katika visiwa vya Unguja na Pemba; Umefika wakati sasa, Zanzibar kuacha kujitangaza kama ni kituo cha utalii cha Jua, Mchanga na Bahari yaani ‘S’ tatu (Sea, Sand and Sun) pekee, na badala yake tutumie pia vivutio vya maumbile ya asili na kimazingira [eco-tourism] kiutamaduni, historia, vyakula, dini, na matibabu yetu, ambavyo vinajipambanua na nchi nyengine kwa vile havipatikani popote duniani; hivyo kiuhalisia ndivyo vivutio vikubwa, na bila shaka tutavutia watalii wengi zaidi”.
Akisisitiza juu ya mchango wa Sekta hiyo, Mheshimiwa Othman amesema kwa mujibu wa Utafiti wa Kumurika Mchango wa Utalii katika Uchumi wa Zanzibar (Zanzibar Tourism Satellite Account ‘TSA’ (Mwaka 2019), ulioendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na Kamisheni ya Maendeleo ya Kimataifa kwa Africa (UNECA), ilionekana kwamba Utalii unachangia asilimia 29.2 ya Pato la Taifa kwa Zanzibar, ambazo bado hazikuweza kufikiwa na sekta nyengine yoyote ya uzalishaji hapa Nchini.
Mheshimiwa Othman amefahamisha kuwa hatua ya kufikiria upya Sekta ya Utalii, itafanikisha mwelekeo wa kwenda na wakati, ikizingatiwa kwamba utalii umepita katika kipindi kigumu cha duniani kote.
Amesema pamoja na changamoto nyingine za kiuchumi, bali utalii wa dunia, Zanzibar ikiwemo ndani yake, kwa kiasi kikubwa, ulielemewa na Janga la CORONA (UVIKO-19), na kwamba kunahitajika njia muafaka na mbadala za kuiendesha sekta hiyo hivi sasa, ili kujikwamua kwa haraka, kutoka pahala pazito ambapo ulimwengu wote upo au umepitia.
Hivyo amesema kutafakri upya juu ya mwelekeo huo, sambamba na Maadhimisho ya Mwaka huu ambayo Kauli-mbiu yake ni ‘Rethinking Tourism’ yaani ‘Kufikiria Upya Utalii’, ni jambo kubwa na lenye umuhimu wa pekee kwa Zanzibar, Tanzania na Afrika yote, kwani hiyo ni Sekta-Kiongozi kwa maendeleo ya uchumi.
Akiongelea juu ya haja ya mashirikiano ya kisekta na kujumuisha kada nyengine za maendeleo na uzalishaji, Mheshimiwa Othman amesema, “kwanza ni jambo lisilo na ubishi kwamba Sekta ya utalii ni mtambuka; maendeleo ya utalii yanaendana na maendeleo ya takriban kila sekta; miongoni mwa sekta muhimu ni pamoja ya usafiri wa anga, usafirishaji wa baharini na nchi kavu, Sekta ya kilimo, viwanda na uzalishaji bidhaa mbali mbali, sekta ya fedha na bima na sekta ya huduma ni wafaidika wakubwa wa maendeleo ya utalii”.
Naye waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe. Simai Mohammed Said amesema kwamba kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa utalii wataendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kukuza sekta ya Utalii Zanzibar ili ulete tija zaidi kwa taifa.
Viongozi na Watendaji, Wawekezaji na Wadau mbali mbali wa Sekta ya Utalii Nchini, wamejumuika katika Kongamano hilo, ambao ni pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrik Ramadhan Soraga; Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Bw. Aboud Suleiman Jumbe; Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima (ZNCCA), Bw. Ali Amour; na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Utalii Zanzibar, Bw. Rahim Bhaloo.
0 Comments