Washiriki wakiendelea na mafunzo |
Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Said Yussuf Kombo akiendesha mafunzo |
Washiriki baada ya kukabidhiwa vyeti |
KATIBU tawala wilaya ndogo ya Kojani Makame Khamis Makame, akizungumza na washiriki wakati wa ufungaji wa mafunzo. |
KATIBU tawala wilaya ndogo ya Kojani Makame Khamis Makame, akimkabidhi cheti cha ushiriki wa mafunzo mmoja wa washiriki wa mafunzo. |
Washiriki wakiwa wameshakabidhiwa vyeti vyao. |
Na Mwandishi wetu.
KATIBU tawala wilaya ndogo ya Kojani Makame Khamis Makame, amewataka mabini na mabwana shamba waliopatiwa mafunzo maalum ya taaluma juu ya namna ya uendeshaji wa shama darasa kupitia mradi wa Viungo kuhakikisha wanafikisha elimu kwa wakulima wote waliotayari kujishughulisha na shughuli hizo ili kuweza kufanikisha malengo ya mradi huo kwa wakulima.
Akizungumza katika
hafra ya kufunga mafunzo ya siku tano kwa wataalam wa kilimo 42 kutoka kwenye
Shehia zote za Pemba ambazo mradi huo unatekelezwa, katibu huyo amesema ili
kufikia malengo ya kuwainua wakulima kiuchumi ni lazima kuwa waangalifu wakati
wa kuchagua wakulima wa kusaidiwa kupitia mradi huo.
Alisema mradi huo kupitia
mpango wake wa utoaji wa elimu ya shamba darasa kwa wakulima itawasaidia
kuondokana na uzalishaji wa mazoea na badala yake kuzalisha mazao kwa kutumia
zana za kisasa na hatimaye kuongeza tija kwa kuzalisha mazao bora na kwa wingi.
“Tunapokwenda
kwenye utekelezaji, twende na watu ambao wapo tayari. Si kwa misingi kwamba
huyu ni mtoto wa bwana shamba, hatutaki. Tunataka wakulima ambao wamejitoa
wenyewe kwa ridhaa zao kwamba ni wakulima ili tuone kwamba mradi huu kweli
mwisho wa siku unaleta tija kwa wakulima wetu kuongeza vipato vyao,” alisema.
Aidha alisema
Serikali za Wilaya na Mkoa zitaendelea kufanya ufuatiliaji wa karibu katika
ngazi ya shehia ili kujiridhisha na utekelezaji wa mradi huo kwa wakulima kwa
lengo la kusaidia ufanisi na utekelezaji wa malengo ya mradi huo.
Alisema, “kwa niaba
ya ofisi ya mkuu wa Wilaya kupitia
wizara ambayo ni mdau ya Tawala za mikoa, katika hili naahidi kwamba tutakuwa
pamoja huko kwenye saiti kuanzia masheha wetu,
lazima tupite kukagua kuona kama shughuli zinaenda kama zilivyopangwa
kwani wakulima nao muda mwingine wanakuwa wababaishaji.”
Aliongeza, “Wananchi
wetu wamezoea kuona miradi mingi inakuwa hai pae inapokuwa katika kipindi cha
utekelezaji na inapomaliza muda wake wanarudi nyuma. Hili hatutaki lijitokeze
katika mradi huu wa viungo.”
Mapema meneja wa
mradi huo, Sharif Maalim Hamad alisema mafunzo hayo yametolewa kwa lengo la
kuwapatia taaluma juu ya namna ya uendeshaji wa shamba darasa ili kurahisisha
ufikiaji wa lengo la mradi kwa kuwafikia wakulima 10,500 kwa upande wa Pemba.
Alisema kutokana na
mradi kuhitaji kufikia idadi kubwa ya wakulima katika utekelezaji wake,
wataalamu hao watatumia mbinu walizofundishwa kuwafikia wakulima hao kupitia
mfumo wa shamba darasa ili matokeo yaweze kupatikana kwa haraka zaidi.
“Mafunzo haya lengo
letu kubwa ni kuwapa taaluma juu ya namna ya uendeshaji wa skuli za wakulima.
Kwasababu shughuli za wakulima ndio kitu muhimu katika utekelezaji wa mradi
huu, wataalam wa CFP pekee yao hawataweza kuwafikia wakulima 21,000 kwa unguja
na pemba kwa hivyo tukaona tuwashirikishe hawa ili tugawiane maeneo ili lengo
la mradi lifanikiwe,” alisema.
Mwezeshaji wa
mafunzo hayo, Said Yussuf Kombo alibainisha kuwa katika mafunzo hayo mada
mbalimbali zimefundishwa ikwa ni pamoja na dhana ya shamba darasa pamoja na
mbinu za Uchunguzi wa mazao shambani (UMASHA).
Alisema, “wataalamu
hawa tumewakumbusha zaidi kuhusu misingi ya utoaji wa elimu kwa wakulima kupitia
shamba darasa ambapo pia wameweza kujifunza kwa vitendo mbinu za uchunguzi wa
mazao shambani (UMASHA) lengo likiwa ni kuwasaidia wakulima kufanya tafiti
ndogondogo za mazao yao.”
Mshiriki wa
mafunzo, Sabra Hamad Ali alisema kutolewa kwa mafunzo hayo yatawawezesha
kufikisha elimu kwa wakulima katika njia ambayo ni rahisi na kwa wakati
kutokana na sahihi kulingana na mazingira ya wakulima wenyewe.
“Tunashukuru sasa
tumepata taaluma mpya na mbinu zaidi za kwenda kuwafundisha wakulima wetu
kupitia shamba darasa, sasa tunakwenda kufanya kazi,” alisema.
Katika mafunzo hayo
washiriki walibidhiwa hati za vyeti vya ushiriki ikiwa ni miongoni mwa hatua za
kutambua ushiriki wao kikamilifu na utayari wa kuanza kutekeleza majukumu yao
ili kufanikisha malengo ya mradi.
Mafunzo hayo ni sehemu
ya utekelezaji wa mradi wa viungo, mboga
na matunda unaotekelezwa Zanzibar na taaasisi za People’s Development Forum
(PDF), Community Forests Pemba (CFP) na Chama cha Waandishi wa Habari wanawake
Tanzania, Zanzibar (TAMWA Zanzibar) kupitia ufadhili wa Umoja wa Ulaya.
0 Comments