HABARI MPYA

6/recent/ticker-posts

KAMPENI 'ONGEA NA KAMANDA' YAFIKIA WANANCHI WA WANGING'OMBE


NJOMBE

Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Wanging'ombe mkoani Njombe, Mrakibu wa Polisi, SP Paul Chiluli amewataka wananchi kuzitambua haki zao pamoja na kutimiza wajibu kwa kuripoti matukio yote ambayo ni kinyume cha sheria ili hatua zichukuliwe kwa wakati. 

Ametoa wito huo wakati wa mkutano na wananchi wa kijiji cha Itambo, kata ya Mdandu wilayani humo ikiwa ni utekelezaji kampeni ya 'ONGEA NA KAMANDA' kwa lengo la kusikiliza kero za wananchi. 


Ameleza kuwa wanachi kutambua haki zao ni msingi muhimu wa kutimiza wajibu katika kushirikiana na jeshi la Polisi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu. 


Akijibu swali kuhusu usahihi wa mwananchi kuchangia pesa ya mafuta kwa askari kwenda kumkamata mtuhumiwa, SP Chiluli ameeleza kuwa askari hawaruhusiwi kudai wala kupokea pesa kutoka kwa wananchi kwa ajili ya mafuta au huduma nyingine wanapokwenda kukamata.


Ameongeza kuwa gharama za kiutendaji za Jeshi la Polisi hubebwa na Serikali , hivyo mwananchi anayeombwa pesa anashauriwa kutoa taarifa mara moja kwa uongozi wa kituo au kwa Kamanda ili hatua zichukuliwe.


Aidha amehimiza kuwa kila raia anapofika kituo cha Polisi anastahili kuhudumiwa kwa wakati, bila upendeleo, bila kuombwa rushwa na bila usumbufu wala kuzungushwa.


Mkutano huo wa kampeni ya "Ongea na Kamanda" umebebwa na ujumbe wa jua haki zako, timiza wajibu wako na toa taarifa za uhalifu na wahalifu kwa wakati kituo cha polisi kilicho karibu nawe.

Post a Comment

0 Comments