HABARI MPYA

6/recent/ticker-posts

WANANCHI NJOMBE WATAKIWA KULINDA NA KUTUNZA AMANI YA NCHI


Na mwandishi wetu 

Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Njombe, Mrakibu Msaidizi wa Polisi ASP Haruna Mtove, amewataka wananchi wilayani humo kuendelea kulinda na kutunza amani iliyopo nchini ili kuwezesha shughuli za maendeleo kuendelea kufanyika bila kikwazo.

Wito huo umetolewa wakati wa mkutano wa uelimishaji jamii kuhusu utii wa sheria bila shuruti uliofanyika katika Kata ya Mjimwema, wilayani humo ambapo amesisitiza kuwa amani ndiyo msingi mkuu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, na kwamba wajibu wa kuilinda haupo mikononi mwa vyombo vya ulinzi na usalama pekee, bali ni jukumu la kila mwananchi.

Ameeleza kuwa kufuata sheria na misingi ya nchi bila kushurutishwa ni njia bora zaidi ya kuzuia migogoro, uhalifu na uvunjifu wa amani katika jamii. 

"Amani tuliyonayo ndiyo nguzo kuu inayotuwezesha kufanya shughuli zetu za kila siku kwa utulivu. Kila mwananchi anapaswa kuwa mlinzi wa mwenzake na kuhakikisha anazingatia utii wa sheria bila kusubiri nguvu ya Dola itumike," alisema  ASP Mtove.

Kwa upande wake Polisi kata ya Mjimwema, mkaguzi wa Polisi INSP  Alexander Makwasa amesisitiza umuhimu wa kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi katika ngazi za mitaa na vitongoji ili kubaini mapema  viashiria vya uhalifu na kuvitokomeza.


Aidha amewasihi wananchi kuendeleza ushirikiano wa karibu na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za haraka na za siri pindi wanapowatilia shaka watu au matendo yanayoweza kuhatarisha usalama katika maeneo yao.

 

Kufuatia elimu hiyo, wananchi wamelishukuru jeshi la Polisi mkoani Njombe kwa kuendelea kuwa karibu nao kupitia elimu mbalimbali na kueleza kuwa elimu hizo zimewasaidia kutambua namna ya kukalibiana na uhalifu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uhalifu kwa jeshi la Polisi bila woga.

Post a Comment

0 Comments