![]() |
Bomba la Maji safi na salama ambalo limekatwa kwaajili ya ujenzi wa barabara na kupelekea ukosefu wa huduma hiyo katika maeneo ya Kilimani, Maisara na maeneo ya Michenzani jumba namba kumi, Unguja. |
Na Mwandishi wetu Zanzibar
Naibu Waziri wa Maji,
Nishati na Madini, Zanzibar Mhe.Shaaban Ali Othman amesema wizara hiyo kupitia
taasisi yake Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) wanajipanga kusambaza huduma ya
maji safi na salama kwa njia ya gari la maji katika maeneo ambayo wananchi wamekosa
huduma hiyo ikiwemo eneo la Kilimani, Maisara, Michenzani jumba (block) namba
kumi n.k.
Kauli hiyo imekuja
kufuatia malalamiko ya wananchi wa maeneo
hayo kulalamikia ukosefu wa huduma hiyo tangu kuanza kwa ujenzi wa Mradi
wa barabara ya Mnazi mmoja hadi Uwanja
wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Unguja.
Akizungumza katika ziara
maalumu iliyoandaliwa jana na Wizara yake katika eneo hilo la mradi wa barabara
hiyo, Mhe, Othman amesema katika kipindi hichi atahakikisha ZAWA wanawafikishia wananchi huduma hiyo kwa njia ya gari la maji
bila ya kuwatoza fedha.
“Tutatoa maji bure katika
kipindi hichi,narudia tena bure kwa maana ya bure hatutomchangisha mtu pesa,
maji tunayo na magari yapo. kwani wizara zote mbili zinafanya kazi kwa
mashirikiano makubwa na muda sio mrefu huduma ya maji itarudi kama kawaida,
hivyo tutasambaza maji bure” Alisema Othman.
Naye katibu Mkuu wa
wizara hiyo Joseph Kilangi amesema ukosefu wa huduma ya maji safi na salama
katika maeneo hayo umetokana na kuathirika kwa miundombinu ya maji wakati mradi
wa barabara ukiendelea hivyo kupitia ziara hiyo imelenga kutafuta majibu ya kujua
wapi mabomba ya maji yatapitishwa ili huduma hiyo irudishwe kwa wananchi.
Amesema wizara yake
imekubaliana na Wizara ya Mawasiliano na Ujenzi kupitisha mabomba ya maji
pembezoni mwa barabara (walk way) hivyo, muda sio mrefu mradi huo utakamilika na
huduma ya maji itarudishwa kwa wananchi kama kawaida.
Aidha katibu Mkuu Kilangi amewaomba radhi wananchi waliyokosa huduma ya maji safi na salama katika kipindi hichi kwani Serikali ya Mapinduzni Zanzibar (SMZ) imejikita katika kuwaletea maendeleo wananchi wake hivyo Barabara ni muhimu na maji ni muhimu kwa maendeleo ya nchi na wananchi wake.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu
Wizara ya Mawasiliano na Ujenzi Khadija Khamis Rajab amesema wizara yake
inafanya kazi kwa mashirika makubwa na Wizara ya Maji, Nishati na Madini hiyo
watahakikisha wanarudisha miundombinu ya maji na umeme yote iliyoathirika
wakati wa ujenzi wa barabara.
Pia amesema miundombinu
ya umeme itakayoathirika itarudisha na taasisi husika Shirika la Umeme Zanzibar
(ZECO) ili wananchi waendelee na harakati zao za maisha ya kila siku.
Wakati huo huo, akizungumza
Mkurugenzi Mkuu ZAWA Mhandisi Dkt. Salha amesema maji yamejaa tele katika tangi
la maji la Mnara wa mbao Kilimani, lakini hakuna jinsi ya kuwafikishia wananchi kutokana na miundombinu ya
maji kuathirika, hivyo taasisi yake inajipanga kuwafikishwa wananchi huduma hiyo
kama walivyotoa katika kipindi cha Mwezi mtukufu wa Ramadhani.
“Taasisi yangu imeshatoa
maelekezo dizaini na dayamita (design na diameter) ya mabomba ya maji ambayo Wizara
ya Mawasiliano na Ujenzi watalazimika kununua kwaajili ya kurudisha huduma hiyo kwa
wananchi kama kawaida” Alisema Mhadis Dkt Salha.
Kwa upande wa wananchi akizungumza
Mkaazi wa Kilimani Bi Luluwa Salum Ali (36) ameiomba Serikali mara tu mradi wa
barabara utakapo kamilika warudishiwe huduma hiyo kwani hivi sasa wanalazimika
kununua gari la maji kwa bei ya Tsh. 15,000 kwa kujaziwa tangi la lita 1500 au
kwenda kukaa foleni kwa jirani ambaye amechimba
kisima huko bei ya kujaziwa tangi la
maji la lita 1500 bei ni Tsh. 5000, lakini watu ni wengi lazima mtu apange
foleni.
“Siwezi kuilamu Serikali najua tunatengenezewa barabara lakini ninachokiomba kwa mamlaka husika barabara itakapokamilika tu, basi turudishiwa huduma hiyo kwani tumekabiliwa na kipindi kigumu hasa ukiangaliwa tofauti ya kipato kwa wananchi” Alisema Luluwa.
0 Comments