TAASISI zinazotekeleza miradi ya kilimo Zanzibar chini ya mpango wa AGRICONNECT Tanzania unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) zimetakiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa shughuli za miradi ili kuchochea ufikiaji wa malengo ya kukuza mnyororo wa thamani kawenye mazao ya Viungo, Mboga na matunda nchini.
Ushauri huo umetolewa kufuatia ziara ya maafisa wa Wizara ya
kilimo na ujumbe kutoka Umoja wa Ulaya iliyofanyika hivi karibuni Unguja na
Pemba kutembelea wanufaika wa miradi hiyo kufanya tathimini ya maendeleo ya
utekelezaji miradi hiyo.
Katibu mkuu Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na
Mifugo Zanzibar, Seif Shaban alipongeza juhudi zinazofanywa na program ya
AGRICONNECT kuinua sekta ya kilimo Zanzibar na kusema utekelezaji wake umeanza
kuzaa matokeo chanya kwa wakulima kuzalisha kwa kufuata mbinu bora za kilimo.
Aliongeza kupitia miradi hiyo ambayo inakuza uchumi wa
wananchi, inaisaidia serikali kufikia lengo lake la kupunguza umasikini kwa
wananchi wake na kuongeza fursa za ajira kwa vijana kupitia shughuli za kilimo.
Alieleza serikali kupitia wizara ya kilimo itaendelea
kushirikiana na wadau wa miradi hiyo ili kuhakikisha changamoto zinazojitokeza
zinatatuliwa kwa wakati na wakulima wanapata fursa ya kuzalisha kwa wingi mazao
bila kikwazo na kukuza uchumi wao na taifa.
Kwa upande wake afisa kutoka Umoja wa Ulaya, Anna
Constantini, alishauri mradi kushirikiana na wakulima kufanyia kazi upatikanaji
wa mfumo wa kisasa wa masoko ili kuwawezesha wakulima kupata taarifa za masoko
kwa njia ya kidijitali.
Amesema mfumo huo ukianza kufanya kazi utawasaidia wakulima
kujua bei za mazao sokoni kupitia simu zao na kuondokana na uuzaji wa bidhaa
kwa bei ya hasara kutokana na kukosekana kwa taarifa sahihi za masoko.
“Lazima mfumo wa masoko ufanye kazi ili kuwawezesha wakulima
kujua nani wa kumuuzia bidhaa zao na wauze kwa bei nzuri ili kujikwamua
kiuchumi,” alieleza Anna Costantini, afisa kutoka Umoja wa Ulaya (EU).
Mapema, Pili Kashinje Ali, mkulima kiongozi na msarifu wa
mazao ya Viungo katika Shehia ya Mahonda, ambaye ni mnufaika wa mradi wa VIUNGO
alishukuru uwepo wa mradi huo na kueleza kuwa umesaidia kurejesha matumaini ya
wakulima kuwekeza katika kilimo.
Alisema, "mwanzo tulikuwa na changamoto ya kukosa
mashine maalumu ya kusaga Viungo, lakini mradi tayari umetuletea mashine hiyo
ambayo sasa inakwenda kuturahisishia kazi na kutuwezesha kuziongezea thamani
zaidi bidhaa zetu ili kupata soko la uhakika kuliko kuuza kama mazao ya kawaida
jambo ambalo linapelekea kuuza kwa bei ya hasara.
Nae Yasin Swalehe Kuhaka, miongoni mwa vijana walionufaika na
utekelezaji wa mradi huo alieleza uwepo wa mradi wa ACRICONNECT umehamasisha
vijana kuona fursa ya kujiingiza katika kilimo na kuondokana na dhana mbaya
kuhusu shughuli za kilimo.
Anaeleza, "baada ya kuhitimu elimu yangu ya chuo
nilikuwa sina mwelekeo kama kijana, lakini kutokana na kukaa mtaani bila kazi
niliamua kuingia katika kilimo baada ya kuhamasishwa na kiongozi wangu Pili
Kashinje ambaye ni mzoefu katika kilimo alinishika mkono na kunielekeza kila
hatua, na nashukuru baadae nilipata fursa ya kufikiwa na mradi huu wa AGRICONNECT
ambao umenisaidia kuona thamani ya kilimo."
Katika ziara hiyo, wanufaika wa mradi wa VIUNGO unaotekelezwa kwa Mashirikiano na People’s Development Forum,(PDF), Community Forests Pemba (CFP), na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) walitembelewa na kuainisha changamoto zinazowakabili wakulima hao.
1 Comments
hakika kabisa imesaidia sana
ReplyDelete