Na mwandishi wetu
Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) na Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) zimesikitishwa kwa
vitendo vya mauaji ya kikatili dhidi ya wanawake wawili yaliyotokea hivi
karibuni Bububu Kijichi na Mbuzini Wilaya ya Maghari “A” Mkoa wa Mjini Magharibi
Unguja.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa
jumapili mei 28 kwa kusainiwa na Mkurugenzi wa ZAFELA, Jamila Mahmoud pamoja na
Mkurugenzi wa TAMWA ZNZ Dkt. Mzuri Issa, imeeleza kwa mujibu wa taarifa
zilizotolewa na vyombo vya habari pamoja na jeshi la polisi, ni kwamba wanawake
hawa wawili, Laura Msemwa (23) na Khairat Juma Bakari (28) wameuwawa kikatili na
watu wasiojulikana.
Taarifa zinaeleza kwamba mauaji hayo yaliyobainika tarehe
20/05/2023 yalifanyika karibu ndani ya wiki moja iliyopita na hivyo kuleta
wasiwai kwa jamii ya wanawake na wasichana.
“ZAFELA na TAMWA, ZNZ
zinasikitika kwamba kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la polisi iliyotolewa hivi
karibuni kwa waandishi wa habari tarehe 25/5/2023 wauwaji wa wahanga hao bado
hawajapatikana.”
Hivyo, Asasi hizo za kiraia zinaliomba sana Jeshi la Polisi
kutumia raslimali zake zote kuwatafuta na kuharakisha upelelezi ili kuwafikisha
watuhumiwa katika vyombo vya sheria mapema iwezekanavyo na hivyo kulipia makosa
yao hayo.
“Kupatikana kwa haki kutawatisha wahalifu wengine ambao wana
nia ya kufanya vitendo hivyo vya kikatili na kuhakikisha kwamba matukio kama
haya hayaendelei kutokea Zanzibar.”
Pia TAMWA -ZNZ na ZAFELA zinaiasa jamii kuacha kutenda
vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambavyo vinakiuka haki za
kibinaadamu na kuteteresha ustawi kwa makundi ya wanawake na wasichana.
Kwa mujibu rikodi za taaisi hizo tokea mwaka 2016, matukio 23
ya mauwaji ya wanawake na watoto yameripotiwa ambapo upatikanaji wa haki
umekuwa ni mgumu kufikiwa.
Tunaamini kwa nchi ndogo kama Zanzibar kukiwepo na upelelezi
na mashirikiano mazuri ya jamii wahalifu wanaweza kupatikana kwa muda muafaka.
0 Comments