Na Mwandishi wetu
Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania,
Zanzibar (TAMWA ZNZ) kitaadhimisha siku ya wanawake dunia tarehe 15/3/2023 kwa
kuandaa kongamano litakalojadili masuala ya matumizi sahihi ya teknolojia,
changamoto na faida zake kwa wanawake na jamii kwa ujumla, sambamba na kuangalia
umuhimu wa matumizi ya kiteknolojia katika taasisi za sheria ili kuharakisha
upatikanaji wa haki.
Hafla hiyo itafanyika katika ukumbi wa Umoja wa Watu
wenye Ulemavu Zanzibar (UWZ) uliopo Kikwajuni kuanzia saa 2:30 asubuhi ambapo
itahusisha washiriki muhimu kutoka katika taasisi za kiserikali na zisizo za
kiserikali ambazo zinajihusisha na masuala ya kisheria, haki za binadamu, elimu
na wanamtandao wa kupinga vitendo vya udhalilishaji.
Matumizi ya teknolojia kwa taasisi zinazo simamia
sheria yatasaidia kurahisisha upatikanaji wa haki kwani yatawezesha kufanyika upelelezi
na kukusanya ushahidi kwa njia mbalimbali, kama ilivyoelezwa katika sheria ya
ushahidi Na.9 ya mwaka 2016.
Sehemu ya tatu kifungu Na. 16 cha sheria hiyo
kinaeleza mbele ya Mahakama ushahidi wa kieletroniki unakubalika “Kukubali
maana yake ni, maelezo ya mdomo au maandishi au yaliyomo katika mfumo wa
kieletroniki, ambayo yanatoa muelekeo katika hoja inayobishaniwa au hoja
inayohusika na ambayo imefanywa na watu wa aina yoyote na katika mazingira
yaliyotajwa.”
Katika kifungu 42
katika mienendo ya kesi za jinai kifungu kidogo cha (a),(b)na(c) vinaelezea
ushahidi wa kielotroniki, kifungu kidogo (a) kinaeleza kuwa “taarifa zilizopatikana
kutoka katika mfumo wa kompyuta, mitandao au mfumo wa kuhifadhia taarifa yatakubaliwa
katika ushahidi”. wakati kifungu kidogo (b) kinaeleza kuwa “kumbukumbu
zilizopatikana kupitia uchunguzi kwa njia za kulinda taarifa zinazojumuisha
mashine ya barua pepe, uwasilishaji wa kielektroniki,” (c) mfumo wa kurikodi
matukio ya sauti au ya picha au tabia au mazungumzo ya watu walioshtakiwa,
yatakubaliwa katika ushahidi.
Aidha, TAMWA ZNZ inatoa wito kwa taasisi zote
zinazosimamia vitendo vya udhalilishaji kuhakikisha miundombinu inaimarishwa na
kuwa ya kisasa zaidi ili kuwezesha matumizi ya kiteknolojia yatakayorahisisha
upatikanai wa haki na kwa wakati. Moja ya agenda kuu ya serikali zote mbili ni
suala zima la haki jinai ambalo ndio msingi mkuu wa utawala wa sheria na
upatikanaji wa haki.
Matumizi sahihi ya teknolojia ya kisasa yatarahisisha
uwajibikaji na upatikanaji haki ili kuwajengea imani wananchi.
Wakati dunia ikiadhimisha siku ya wanawake duniani jamii
inapaswa kuelewa umuhimu wa wanawake unaoenda sambamba na matumizi sahihi ya
teknolojia yatakayoleta maendelo kwa wote na kufikia uwiano wa kijinsia na sio
matumizi yatakayochangia kuendeleza udhalilishaji na ukatili.
Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani huadhimishwa
kila mwaka ifikapo tarehe 8 Machi ikiwa na lengo la kutoa fursa kwa wanawake,
taasisi za kiserikali na asasi za kiraia na wadau mbalimbali kupata fursa ya
kukaa pamoja kujadili mafanikio na changamoto zinazomkabili mwanamke katika
jamii na pia kutafakari jinsi ya kuyafikia malengo ya maendeleo endelevu
ifikapo 2030.
Bado kuna changamoto nyingi zinazowaandama wanawake
zikiwemo matumizi yasio sahihi ya teknolojia yanayopelekea kuendeleza vitendo
vya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia hasa kwa wanawake na watoto.
Kauli mbiu ya TAMWA ZNZ mwaka huu ni “Tuhimize mtumizi sahihi ya
kiteknolojia ili yalete uwiano wa kijinsia” Kauli mbiu hii inakwenda sambamba na kauli mbiu ya
kitaifa isemayo “Wekeza Ubunifu na
matumizi sahihi ya Teknolojia kwa usawa wa Kijinsia” ambapo kauli mbiu zote zinasisitiza umuhimu wa
mtumizi sahihi ya teknolojia katika nyaja zote ili kufikia usawa wa kijinsia na
maendeleo endelevu kwa wote.

0 Comments