HABARI MPYA

6/recent/ticker-posts

WANAHARAKATI WAOMBA UIMARISHAJI MIFUMO KESI ZA UDHALILISHAJI

 


Imeandikwa na Gaspary Charles


IKIWA wanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsia Ulimwenguni wanaendelea kuunganisha nguvu kupaza sauti kwa jamii kukomesha ukatili kupitia kampeni ya siku 16, baadhi ya wanaharakati kisiwani Pemba wameshauri kuimarishwa zaidi kwa mifumo muhimu ya usimamizi wa haki ili kuweka uwazi katika kesi hizo.

Wametaja miongoni mwa maeneo ambayo yanahitaji maboresho ni pamoja na uwekaji wa mpango maalum wa kuwatambua mahakimu wanaofanya vizuri katika usimamizi wa kesi na kuwachukulia hatua wale wanaochelewesha kesi kwa makusudi ili kuweka uwajibikaji wa pamoja katika uendeshaji wa kesi.

Wakizungumza na Redio Jamii Micheweni, wanaharakati hao wameeleza kuwa iwapo kutakuwa na mfumo wa kufuatilia utendaji na uwajibikaji wa mahakimu wa kesi hizo utasaidia kupunguza malalamiko ya wananchi juu ya mwenendo wa usimamizi wa kesi hizo.

Nassor Bilali Ali, mmoja wa wanaharakati hao kisiwani Pemba amesema licha ya juhudi kubwa kuchukuliwa na wadau kupambana na udhalilishaji lakini kukosekana kwa mfumo wa kuweka kumbukumbu ya mwenendo wa kesi bado ni miongoni mwa tatizo linalokwamisha taifa kujipima mwelekeo wake katika kupambana na vitendo hivyo.

Ameeleza kwa kuwa msisitizo wa kaulimbiu ya kimataifa mwaka huu inasisitiza wanaharakati wote kuungana pamoja kuhakikisha ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike unakomeshwa, hivyo ameiomba serikali na mamlaka husika kuimarisha mifumo yake ya takwimu za matukio hayo ili zioneshe kwa uwazi mwenendo wa kesi hizo na idadi ya kesi zilizotolewa maamuzi katika kila kipindi ili kutoa mwelekeo halisi wa matukio hayo.

Kwa upande wake Hafidh Abdi, mkurugenzi wa jumuiya ya KUKHAWA, amesema iwapo kutakuwa na mifumo imara inayosimamia uwazi wa takwimu zenye kutoa mchanganuo wa mwenendo na idadi ya kesi zilizochukuliwa hatua na zilizofutwa itachochea uwajibikaji katika kufanikisha juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Husein Ali Mwinyi kuanzisha mahkama maalum ya kesi za udhalilishaji.

Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar, (TAMWA ZNZ) ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa amesema jamii inapaswa kutumia kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili kujitafakari na kupunguza muhali na badala yake iwe msitari wa mbele kuripoti matukio haya kwa wakati pale yanapotokea na kuwa tayari kutoa ushahidi unaohitajika kwenye vyombo vya sheria ili kufanikisha hatua kuchukuliwa dhidi ya watuhumiwa.

Kwa mjibu wa ripoti ya takwimu za ukatili na udhalilishaji wa kijinsia Zanzibar kutoka ofisi ya mtakwimu mkuu wa serikali zanzibar kwa mwezi wa agositi 2022, jumla ya matukio 131 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa mwezi huo ambao waathirika Wanawake ni 12 (asilimia 9.2) na watoto ni 119 sawa na asilimia 90.8, miongoni mwao wasichana walikuwa 84 (asilimia 70.6) na wavulana walikuwa 35 (asilimia 29.4).

Chimbuko la maadhimisho ya Siku 16 za kupinga ukatili kwa wanawake na watoto wa kike linatokana na tamko la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa awamu ya saba Kofi Annan, mwaka 2006 la kuyataka mataifa yote yatambue kuwepo kwa tatizo kubwa la ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto wa kike Duniani.

Post a Comment

1 Comments

  1. Tatizo hata hao wakutoa ripoti ndio wadhalilishaji wenyewe

    ReplyDelete