HABARI MPYA

6/recent/ticker-posts

"SERIKALI BADO INAKIUKA MATAKWA SHERIA YA MTOTO ZANZIBAR "- WADAU

Hakimu wa Mahkama ya mkoa Kusini Pemba, Muumin Ali.

Imeandikwa na Gaspary Charles


WAKATI ulimwengu ukiwa unaendelea kuunganisha pamoja uanaharakati wa kupinga ukatili wa kijinsja kwa wanawake na watoto wa kike katika kampeni ya Siku 16 za kupinga ukatili, imeelezwa kuwa Zanzibar licha ya kuwa na sharia bora inayomlinda mtoto lakini sharia hiyo bado haitekelezwi ipasavyo ili kutoa ulinzi kwa watoto.

Akizungumza na Redio Jamii Micheweni, Hakimu wa Mahkama ya mkoa Kusini Pemba, Muumin Ali amesema kuwa Sheria ya mtoto Zanzibar Na. 9 ya mwaka 2011 inamtaka mtoto baada ya kubainika na makosa apelekwe kwenye chuo maalum (approved schools) kwa muda wa miezi 6 ili arekebishwe tabia.

Amebainisha kuwa licha ya sharia kuweka maagizo hayo lakini bado vyuo hivyo havipo Zanzibar na badala yake mahakama inalazimika kuwapa adhabu ya kulipa fidia ambayo inalipwa na wazazi wa watuhumiwa jambo ambalo halilengi kurekebusha tabia za watoto.

Amesema kutokana na hali hiyo inapelekea jamii kupunguza Imani kwa mahakama baada ya kuona watuhumiwa wengi watoto wakiachiliwa huru baada ya kulipa fidia.

Hakimu Muunin amewataka wadau wa kupambana na vitendo hivyo kutumia siku 16 za kupinga ukatili kwa kuikumbusha serikali juu ya umuhimu wa kujenga vyuo hivyo maalum kwaajili ya watoto waliopatikana na hatia ya makosa kama ambavyo sharia inaelekeza ili vitumike kuwarekebisha tabia na kuondokana na utaratibu wa kuwatoza fidia ambao hupelekea kuongezeka kwa vitendo hivyo.

Mratibu wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa, amesema serikali kushindwa kutekeleza matakwa ya sharia ya mtoto kwa kujenga vyuo hivyo maalum kunatia doa utekelezaji wa sharia hiyo ambayo imetajwa kuwa miongoni mwa sharia bora za kulinda watoto barani Afrika.

Ameiambia redio Jamii Micheweni kuwa ucheleweshaji ujenzi wa vyuo hivyo kunaongeza hatari ya watoto wengi kuharibika zaidi kwa kukosa sehemu sahihi ya kurekebisha tabia zao, hivyo wanaharakati wa haki za watoto wanaendelea kuikumbusha serikali umuhimu wa kujenga vyuo hivyo ili kuhakikisha utekelezaji wa sharia hiyo unaleta mafanikio kwa taifa.

Kwa pande wake Maalim Nassor Mwananchi kutoka Wilaya ya Mkoani amesema kuna haja ya kuongeza elimu ya afya ya uzazi kwa watoto na vijana katika umri wa mapema kwani vitendo vingi vya udhalilishaji kwasasa vinachochewa na watoto kukosa fursa na elimu sahihi ya masuala ya afya ya uzazi.

Nae Awena Salim Kombo, mwanamtandao wa kupinga udhalilishaji mkoa wa Kaskazini Pemba amevitaka vyombo vya sharia kusimamia misingi ya haki katika usimamizi wa kesi kwa kuchukua hatua sawasawa kwa walio na pesa na asiye na pesa pale anapojihisisha na matukio hayo ili kuondoa mkanganyiko kwamba wanaochukuliwa hatua ni wananchi wasio na uwezo pekee.

Kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike huadhimishwa kila ifikapo 25 novemba na kilele chake 10 desemba ya kila mwaka ambapo mwaka 2022 yanabebwa na kaulimbiu inayowahimiza wanaharakati kuunganisha uanaharakati wao kukomesha vitendo hivyo katika jamii.

#SautiYaMicheweni #16DaysofActivism2022#16DaysOfActivism #ukatilihauvumiliki

Post a Comment

1 Comments

  1. Tatizo la serikali yetu viongozi wanajivunia kuwa na sheria bora kwenye makaratasi lakini utekelezaji wake hakuna kitu, Sheria zinatekelezwa kwa matakwa ya kiongozi ndiyomaana kila siku tunajisifia kwamba tuna sheria nzuri lakini uhalisia wake hakuna lolote linalofanyika. Tumerogwa na nani sijui yani.

    ReplyDelete