HABARI MPYA

6/recent/ticker-posts

MTANDAO KUPINGA UKATILI PEMBA UMECHOCHEA KASI MAKABILIANO YA VITENDO HIVYO KWENYE JAMII


Imeandikwa na Gaspary Charles

JUMLA ya matukio 88 ya udhalilishaji Pemba yamefuatiliwa na mtandao wa kupinga udhlilishaji mikoa ya Kaskazini na Kusini Pemba kwa mwaka 2022 ikiwa ni matokeo ya mwendelezo wa harakati za kupambana na vitendo hivyo katika jamii.

Hayo yamebainishwa na wanamtandao hao wakati wakizungumza na Redio Jamii Micheweni kwa nyakati tofauti wakati ambapo wanaharakati duniani wanaendelea na kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike.

Wameiambia redio Jamii Micheweni kuwa kati ya matukio hayo waliyofualia katika ngazi mbalimbali, kwa upande wa mkoa wa kusini Pemba ni matukio ya kesi 26 na kati ya hizo kesi 19 zilihusiana na matukio ya ubakaji, huku mkoa wa Kaskazini Pemba kukiwa ni kesi 62 na kati yake kesi 30 ni za ubakaji.

Mwenyekiti wa mtandao huo mkoa wa Kaskazini Pemba, Rashid Mshamata amesema kati ya kesi 26 zilizofuatiliwa na wanamtandao huo kesi 30 zilihusisha matukio ya ubakaji, shambulio la aibu sita, kunajisi mvulana nane, kuingilia kinyume moja, kumpa mimba mwari matukio matatu, utelekezaji wa watoto kesi moja, ulawiti mbili, kunyimwa haki ya elimu moja pamoja na udhalilishaji mkubwa wa kijinsia moja.

Alieleza, “kati ya hizo, kesi 36 mpaka sasa zipo chini ya upelelezi wa Polisi ambapo kati yake kubaka ni kesi 20, kutorosha msichana 4, shambulio la aibu 4, kunajisi mvulana 1, kumpa mimba mwari 3, utelekezaji 1, ulawiti 2, udhalilishaji mkubwa 1.

Aliongeza kuwa kati ya matukio hayo, kesi Tisa bado zinaendelea Mahakamani, kesi 11 zimeondolewa kwa kukosa ushahidi wa kutosha huku kesi nne zikiwa zimepata hukumu.

Kwa upande wake Shaaban Kassim, mwenyekiti mtandao huo mkoa wa Kusini Pemba alieleza kwa upande wa Mkoani mtandao huo uliopo chini ya Chama cha Waandidhi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) umefatilia jumla ya kesi 26, kati ya hizo kesi za ubakaji ni 19, kulawiti 4, kutorosha 1, utelekezaji 1, kujaribu kubaka na kulawiti 1.

“Mpaka sasa, kati ya kesi 19 za ubakaji tulizofuatilia, kesi 7 zipo polisi, 4 zipo mahakamani, 1 imepata kifungo, huku kesi 4 ziliondolewa mahaakamani kwa kukosa ushahidi wa kutosha na kesi 3 watuhumiwa walitoroka,” Shaaban Kassim, mwanamtandao kupinga udhalilishaji Wilaya ya Mkoani Pemba,” alifahamisha Shaaban.

Alieleza kuwa licha ya juhudi kubwa zinazochukuliwa na mtadao huo kwa kushirikiana na wadau wengine, lakini bado sharia ya mtoto inakwaza mwenendo wa kesi hizo kutokana na licha ya matukio mengi ya udhalilishaji kuwahusisha watoto lakini hakuna adhabu stahiki inayochukuliwa inayolenga kuwarekebisha tabia watoto hao.

Alifahamisha, “kutokana na kushamiri kwa kundi kubwa la watoto kutuhumiwa kuhusika udhalilishaji, ni vyema kuwepo kwa sheria ambayo itawabana watoto wanaojihusisha na matukio haya ili kuwadhibiti zaidi kuliko kuendelea na huu utaratibu ambao hauwabani kwa lengo la kurekebisha tabia zao na badala yake kuishia kutozwa na fidia tu,” Shaban Kassim, mwanamtandao kupinga.

Nae Siti Faki Ali, mwanamtandao kupinga udhalilishaji Kaskazini Pemba, alisema wakati dunia inaadhimisha siku 16 za kupinga ukatili, bado jamii inahitaji elimu zaidi kuhusu kupambana na udhalilishaji hasa elimu ya utoaji wa ushahidi mahakamani kwenye kesi hizo kutokana na kesi nyingi zinafutwa kwa kukosa ushahidi.
Kwa upande wake Haji Shoka, Mwanamtandao kupinga Udhalilishaji Pemba, alishauri kuwepo kwa sharia maalum inayowabana wazazi wanaoshndwa kusimamia malezi bora ya watoto na kupelekea kujiingiza katika vitendo vya udhalilishaji ili wawajibishwe.

“Nashauri kuwepo kwa sheria inayowabana wazazi wanaoshindwa kuwadhibiti watoto wao kwa kuwaacha wakizurura usiku kwasababu wazazi wengi kwasasa wameshindwa kuwadhibiti watoto wao lakini kukiwa na sharia hii itasaidia kuwaepusha watoto na matukio ya udhalilishaji,” Haji Shoka, Mwanamtandao kupinga Udhalilishaji Pemba.”

Zaina Abdalla, mratibu mradi wa kupinga udhalilishaji TAMWA Zanzibar aliwataka wadau kutumia siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike kuungana pamoja kutokomeza vitendo hivyo.

Alieleza, “tukiwa tunaendelea na kampeni yetu ya Siku 16 za kupinga Ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto wa kike, naombeni wadau wote tuungane pamoja kukomesha udhalilishaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto kama ambavyo kaulimbiu ya maadhimisho mwaka huu inatuelekeza.”

Ali Abdulrahman Ali, Hakimu Mahakama mkoa Kaskazini Pemba amesema kutokana na juhudi kubwa zinazochukuliwa na wadau mbalimbali kwenye kesi hizo wakiwemo wanamtandao hao, imeirahisishia mahkama kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufanya mrundikano wa kesi kupungua.

Alieleza kuwa kutokana na juhudi hizo, kesi nyingi kwasasa zinachukua muda mfupi kutolewa hukumu tofauti na mwanzo.
Aidha alibainisha kuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya waathirika kukataa kutoa ushahidi mahkamani hasa kwa kesi zinazowahusu waathirika watoto wa miaka kati ya 14 hadi 17 jambo ambalo linapelekea ugumu katika kesi hizo.

Wakati ambapo dunia inaendelea na kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili kwa wanawake na watoto wa kike, ni jukumu la kila mmoja kuunganisha nguvu na muda wake ili kukomesha vitendo hivyo hatari kwa wanawake na watoto kwenye jamii.

#SautiYaMicheweni #16DaysofActivism2022#16DaysOfActivism #UkatiliHauvumiliki

Post a Comment

1 Comments