HABARI MPYA

6/recent/ticker-posts

KUELEKEA QATAR: NYOTA HAWA ULAYA KULIKOSA KOMBE LA DUNIA QATAR 2022


Imeandikwa na Gaspary Charles.

 

Wakati ambapo joto la Michuano ya Kombe la Dunia la nchini Qatar 2022 likizidi kupanda na wapenzi wa soka ulimwenguni wakisubiri kwa hamu kushudia ubabe ndani ya dakika 90 katika viwanja 8 bora duniani kwa sasa huko Qatar ambapo wababe wa soka ulimwenguni watakutana kupimana uwezo wao.

 

Lakini upande wa pili kwenye mataifa shiriki ya michuano hiyo wasiwasi uzazidi kutanda, na hii ni kutokana na nyota wengi ambao ni tegemeo kuendelea kuandamwa na jinamizi la majeruhi jambo ambalo linaongeza presha ya sintofahamu iwapo kama nyota hao hawatakuwa sehemu ya watakaotua jijini DOHA kutoa burudani kwa wapenzi wa soka ulimwenguni.

 

Michuano hiyo ambayo itaanza kutimua vumbi 20 Novemba. Ni wazi kwamba makocha wa timu za taifa zitakazoshiriki mashindano haya bora na maarufu duniani, kwasasa hofu yao kubwa ni kupoteza nyota wake muhimu kwenye kikosi kuelekea QATAR na hii ni kutokana na kuwa nyota wengi duniani watashiriki mechi za vilabu  vyao hadi wiki moja kabla ya michuano hiyo kuanza.

 

Ikiwa ni wiki chache zimesalia kabla ya macho yote kuelekezwa QATAR, hawa hapa ni baadhi ya nyota ambao kuna uwezekano mkubwa wakakosekana kwenye orodha na kumbukumbu za waliofanya makubwa kwenye ardhi ya kifalme katika michuano hii iliyobeba msisimko mubwa kote duniani.



N'Golo Kante, Kiungo wa kati wa safu ya ulinzi ya Chelsea na Mabingwa watetezi wa kombe hilo UFARANSA chini ya kocha wake Didier Deschamps anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi minne kufuatia upasuaji wa kurekebisha tatizo la misuli ya paja jambo ambalo linamfanya kuwa miongoni mwa nyota ambao tayari imethibitishwa kuwa hatokuwa sehemu ya kikosi cha Ufaransa kitakachoelekea Qatar kutetea ubingwa wake.

Mwingine ni nyota Paul Labile Pogba, Kiungo wa zamani wa Manchester United ambaye mpaka sasa hajacheza mechi yoyote tangu arejee Juventus msimu huu wa joto kufuatia upasuaji wa goti na hii inamfanya kuongeza wasiwasi wa kukosekana kwenye kikosi cha ufaransa kwenye safari ya kusaka ubingwa upya wa michuano hiyo.

Nyota wengine ni pamoja na Reece James ambaye Jeraha la goti alilopata dhidi ya AC Milan inamuacha mchezaji huyo wa Chelsea shaka kuu ya kuungana na kikosi cha England katika michuano hiyo.


Pia nyota wa Bayern Munich Lucas Hernandez, beki wa Manchester City Kyle Walker, John Stones na Harry Maguire wapo katika hatihati ya kurejea kwenye safari ya Qatar na timu ya taifa England na hii ni kutokana na Kyle Walker alikuwa amesalia na wiki sita kupona jeraha lake la kinena huku Stones nyota wa Manchester City na Maguire wa Manchester United wote hawajacheza tangu kupata jeraha la msuli wa paja kwenye mechi ya Ligi ya Mataifa dhidi ya Ujerumani iliosha 3-3 mwezi uliopita.

Mashabiki wa England kwasasa wanakabiliwa na wasiwasi mkubwa katika safu yao ya ulinzi jambo ambalo linazidi kuongeza hofu zaidi kwa meneja Gareth Southgate na benchi lake la ufundi juu ya mstakabali wa kikosi chake kuelekea Qatar.

Kwa upande wa ujerumani pia hali si shwari sana kwani Wasiwasi mkuu kwa Ujerumani unamzunguka nyota na nahodha wa Borussia Dortmund ya nchini humo, Marco Reus 33, aliyejeruhiwa kano za kifundo cha mguu mwezi Septemba. Jeraha ambalo lilimfanya akose ushindi wa Ujerumani wa Kombe la Dunia huko Brazil mnamo 2014.


Pia nyota, Leroy Sane mwenye umri wa miaka 26 alirarua msuli wa paja lake la kushoto wakati Bayern Munich iliposhinda 5-0 dhidi ya Freiburg siku ya Jumapili. Licha ya kuwa mpaka sasa klabu yake haijatoa muda wa kupona kwa Sane, ikisema tu kwamba watamkosa fowadi huyo jambo ambalo linatia tumbo joto mashabiki wa taifa hilo.

Meneja Fernando Santos wa kikosi cha Ureno anaweza kukosa huduma za wachezaji wanne muhimu kwa kampeni yao ya Kundi H dhidi ya miamba ya soka barani afrika Ghana, Korea Kusini na Uruguay.

Nyota hao ni pamoja na Diogo Jota, mshambuliaji wa Liverpool ambaye imethibitika atakosa Kombe la Dunia baada ya kutolewa nje kwa machela akiwa na jeraha la paja katika muda wa nyongeza wa ushindi wao wa 1-0 wa Ligi Kuu ya Uingereza dhidi ya Manchester City mnamo Oktoba 18.

Aidha Uholanzi, ambayo ni mpinzani mkuu wa timu ya taifa ya England, katika kufuzu kwa raundi ya 16 bora, pia itamkosa mchezaji wake tegemeo Georginio Wijnaldum, kiungo wa kati wa zamani wa Liverpool mwenye umri wa miaka 31, aliyecheza mechi 86, alijeruhiwa kwenye mguu wake wa kulia baada ya kucheza mchezo mmoja tu kwa mkopo akiwa Roma.

Kwa upande wake Argentina walioshikilia nafasi ya pili  kwenye kombe la dunia 2014 pia watalazimika kuvumilia bila mchezaji muhimu wa klabu ya Roma Paulo Dybala ambapo mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 atakosa mashindano hayo baada ya kupata jeraha la paja wakati alipokuwa akipiga penalti mapema mwezi  Oktoba.

Pia Argentina wakiwa katika hatihati ya kukosa huduma ya Angel Di Maria Winga wa zamani wa Manchester United ambaye pia alipata jeraha la paja akiwa kwenye majukumu ya Ligi ya Mabingwa akiichezea miamba ya soka Italia, Juventus wiki iliyopita na atakuwa nje kwa wiki tatu, hivyo kumuacha akiendelea kusubiri uharaka wa kupoa kabla ya muda wa kombe la dunia kufika.


Kikosi cha Brazil nacho hakipo salama sana, kwani mchezaji mmoja wa Ligi ya Premia anasalia kuwa mashakani kwa timu ya Brazil inayotaka kushinda Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu 2002, lakini matumaini yao kwasasa yemezidi kurejea kwa Richarlison, mshambuliaji wa Tottenham ambaye awali alionekana akiwa kwenye magongo baada ya kupata jeraha la mguu katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Everton Oktoba 15, lakini sasa meneja wa spurs, Antonio Conte amefufua matumaini ya wabrazil baada ya kusema nyota huyo anapaswa kuwepo kwenye kombe la Dunia baada ya uchunguzi.

Licha ya wasiwasi wote, lakini ukweli ni kwamba timu zote zitalazimika kusubiri hadi wiki ya mwisho ya kuelekea kuanza kwa mashindano haya na hii ni kutokana na ugumu wa ratiba ya michezo ya ligi mbalimbali barani ulaya, ambapo ligi hizo zitaendelea kuchezwa hadi wiki moja kabla michuano kuanza.


Post a Comment

0 Comments