Wataalamu wa sayansi ya jamii wanaamini kwamba uongozi ni rasilimali muhimu ya kuchangiza maendeleo ya jamii na ndiyo sababu nchi za kidemokrasia zinafanya uchaguzi kila baada ya miaka fulani ili kupata viongozi bora.
Katika miaka ya nyuma ilikuwa
siyo rahisi kukuta mtu mwenye
ulemavu anapewa fursa ya kuwa kiongozi.
Lakini baada ya kuanza kupewa jukumu hilo wapo waliothibitisha kwamba wana uwezo mkubwa wa kiuongozi.
Jamila Borafya
Hamza anayeishi Mwanakwerekwe Zanzibar
ni mmoja wa watu wenye ulemavu wa macho, lakini kwa jinsi alivyoshika nafasi
nyingi za uongozi na anavyopambania maslahi ya watu wewe siyo rahisi ukatambua
kwamba ana ulemavu huo.
"Kilichonivutia zaidi kuingia kwenye
uongozi nilikuwa natamani watu waone watu wenye ulemavu tunaweza kuongoza”,
amesema Jamila ambaye ni Mjumbe Baraza la Watendaji Taifa katika Baraza la
Vijana Zanzibar na kuongeza;.
‘’Nilikuwa najiamini na kuamini naweza na
familia ilikuwa inanitia moyo nikawa nazidi kuhisi naweza na kweli nikawa naweza kuongea mbele za watu, nasafiri
sehemu mbali mbali na kutatua kero za watu."
Binadamu bila kujali ana ulemavu au la, hakuna ambaye anaweza
kutekeleza majukumu yake yote bila kutegemea watu wengine.
Jamila anasema, anatekeleza majukumu yake ya kiuongozi
kutokana na msaaada anaoupata kwa watu
anaofanya nao kazi .
Lakini anasisitiza "hata mimi mwenyewe sijajiweka nyuma
,maana natafuta mtu wa kufatana nae maana sheria zinatutaka tutembee na
wasindikizaji, na mimi huwa natekeleza majukumu yangu hata kama hawajaniwezesha
kikamilifu na mwisho hawamini wanachokiona".
MAMBO KUJIVUNIA ALIYOWAFANYIA ANAOWANGOZA
Watu wenye busara husikika wakisema uongozi ni kuacha alama
nzuri kwa wale uliowaongoza au unaoendelea kuwaongoza.
Kuna vitu vingi Jamila amevifanya mpaka sasa kwa vijana
anaowaongoza na vimeweka alama katika
mioyo ya vijana hao.
"Kiongozi Jamila anafanya mambo
makubwa sana ambayo muda mwingine ni vigumu mtu mwenye hali kama yake kufanya
maana, anakwenda masafa marefu kuhudhuria vikao bila ya kujali hali yake,
tunamuamini na vijana wengi sana na tunamsikiliza", amesema Fatawi Habib Khamis mwanachama Baraza
la vijana.
Mjumbe mwingine wa baraza hilo Zainab Mtumwa Ame, anasema "Jamila
anafanya kazi zake za uongozi katika mazingira magumu lakini matokeo yake anachofanya ni mazuri na hutengemei , yuko
mbele kwa kila kitu na anajiamini kueleza shida za vijana hata awe nani anasema
na mwisho wa mazungumzo yake lazima aeleze nini kifanyike ili kutatuwa tatizo
alilowasilisha".
Jamila anasema yeye anamini mambo mengi sana
mazuri huwafanyia watu wanaowaongoza ambayo mpaka sasa yamewacha alama kwenye
maisha yao.
Anasema "
vijana wengi kupitia mimi wamepata ajira kwa kuajiriwa au kujiajiri na hii ni
kutokana na miongozo yangu ninayowapa vijana ninao waongoza na mpaka sasa wengi
wao wananishukuru maana nimewafundisha ujasiri mkubwa sana ".
Pia amesema kuwa wapo vijana kupitia muongozo wake wamepata
fursa nje ya Zanzibar.
CHANGAMOTO KATIKA
UONGOZI WAKE
Kila kazi inachangamoto yake katika utekelezaji na ndo ilivyo
pia kwa Jamila Borafya Hamza. Katika maisha ya uongozi wake licha ya kutekeleza
majukumu yake kwa uweledi mkubwa
anapitia changamoto nyingi sana.
Hata hivyo yeye binafsi haoni ni changamoto, bali anachukuliya hizo changamoto kama ni fursa
kwake.
"Changamoto kubwa
ni ulemavu wa macho, ninapotaka kugombea mtu haniamini anaona yule ataongozaje
lakini anasahau kwamba macho siyo yanayongoza isipokuwa akili na maarifa",
amesema Jamila
Vile vile Jamila ametaja changamoto ya mazingira anayofanyia
kazi sio rafiki na hivyo hupelekea ugumu katika utekelezaji wa majukumu yake ,
akataja rasilimali fedha kuwa pia ni miongoni mwa changamoto.
Kadhalika amesema ingawa anapambana hana vifaa saidizi ndiyo maana baadhi ya
maeneo ushiriki wake unakuwa mdogo.
ANAVYOTATUA CHANGAMOTO
Mshairi moja aliwahi kusema
"mwenye mapenzi haoni ingawa
anayomacho". Changamoto
hizo Jamila kwake haoni kama ni kikwazo cha kwamba yeye asitekeleze majukumu
yake. Badala yake anazitatua changamoto
hizi kwa kujiamini na kupambana kwa kila hali.
"Ukiwa kiongozi na ukiwa unajiamini
lazima uwe na ushawishi mzuri kwa vijana au kwa wale unaowaongoza”, anasema
Jamila na kuongeza:
“Maana wale ninaowaongoza ushawishi wangu na utamu wa maneno
yangu wanakuwa wanakubali na pia tunatatuwa changamoto hizi kwa kupambana na
kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi zaidi’’.
MAZUNGUMZO NA BABA YAKE
Jamila ni kijana anayeishi na wazazi wake wote wawili baba na
mama. Mwandishi wa makala hii ameamuwa kukaa chini na baba mzazi wa Jamila na
kutaka kujuwa mengi kuhusu mtoto wake, tangu utoto wake mpaka kukua na haswa
katika uongozi.
Baba mzazi wa Jamila
mzee Borafya Hamza amesema Jamila alizaliwa akiwa na ulemavu wa macho
lakini uwezo wake wa kuongoza.
“Sisi wazazi
tulianza kuona uhodari wake tangu
akiwa mtoto mdogo sana maana alipokuwa akicheza na watoto wenziwe alipenda
kuigiza kama mama, na hata shuleni alipenda uongozi na kuanza kuchaguliwa
nafasi mbali mbali’’.
Amesema baada ya kugundua
uwezo wa kuongoza alionao mtoto wao
walianza kuchukuwa hatua ya kukuza kipaji chake kwa kumsaidia kwa hali
na mali mpaka hapa alipofikia.
"Tulianza
kumsaidia kwa kumtiya moyo, kujitahidi kumsomesha na kwa sasa ili aweze kutekeleza majuku yake
ya uongozi vizuri ", alisema mzee Borafya Hamza
Mzee Hamza amewaasa wazazi wenye watoto wenye ulemavu ambao wana vipaji kwamba, wasiwalemaze watoto wao badala
yake kuwaunga mkono kwa vipaji
walivyonavyo na kuwachanganya kwa watoto weziwao, ili akili zao zitanuke na
wajione kama binadamu wengine.
MWANZO WA UONGOZI WAKE
MPAKA SASA
Safari ya Jamila
katika uongozi ilianza rasmi mwaka 2012
ambapo amesema ‘’nilikuwa waziri wa habari katika serikali ya
wanafunzi ya skuli ya Kisiwandui msingi ‘’.
Amesema baada ya hapo alisitisha
kuendeleya na uongozi mpaka alipoingia sekondari ambapo mwaka 2015 alijiunga na
club ya TUSEME ndani ya skuli yao Haile Thalasi.
Amesema mwaka 2016
alingia ndani ya BUNGE LA VIJANA ZANZIBAR baada ya kushida katika uchaguzi na
alikuwa ni mjumbe wa kawaida na kuongeza:
“Mwaka huo huo nikawa
mwenyekiti Baraza la Vijana shehia ya Mwanakwerekwe na baadae kuwa mjumbe wa kamati tendaji wilaya ya magharib B Baraza la vijana Zanzibar”
Kwa mujibu wa Jamila,
mwaka 2017 alichaguliwa kuwa mwenyekiti
wa jumuiya ya wasiona Zanzibar katika ngazi ya
wilaya. Mwaka 2018 akawa mwenyekiti
kamati ya vijana michezo katika Baraza la vijana Zanzibar.
“Mwaka, 2018 nilirudi
tena Bunge la vijana Zanzibar na
kuchaguliwa Waziri wa Maendeleo ya Vijana Zanzibar’’ amedokeza .
Jamila amesema aliingia rasmi kwenye siasa mwaka 2019
na kuchaguliwa mjumbe wa kamati tekelezaji tawi, ambapo mwaka 2020
aliteuliwa kuwa mjumbe wa kamati ya kupinga vitendo vya udhalilishaji shehia ya
Mwanakwerekwe akiwakilisha vijana na watu wenye ulemavu.
Mwaka 2020 pia aligombea uwakilishi katika jimbo la
Mwanakwerekwe na mwenyewe anasema ‘’ sikutaka kuanza na viti maluum, lakini
katika uchaguzi huo sikufanikiwa kushinda’’.
Hata hivyo amesema
mwaka 2021 alitoka wilaya kwenda taifa Baraza la vijana kugombania nafasi ya ujumbe baraza la
watendaji taifa na akashinda, kwa sasa ndio cheo anachotumikia.
VIONGOZI CHIPUKIZI.
Baadhi ya viongozi chipukizi
wanawake Zanzibar nao wamesema, wanjifunza vitu vingi sanaa kutokana na
ujasiri na moyo wa kizalendo alionao Jamila katika uongozi wake.
Mwajuma Zaidi Makame
ni kiongozi chipukizi amesema, "Anajifunza vitu vingi sanaa kupitia kiongozi Jamila na kwamba ni mfano wa
kuigwa na jamii haswa vijana wakike kama sisi ambao ndo kwanza tunachipukia
katika uongozi"
Rayyan Makame Abdallah, yeye anasema kwa Jamila
ananjifunza kwamba “Ni muhimu kujitolea
kwa wale unaowaongoza”.
Jamila mwenyewe anatoa ushauri kwa vijana wanawake viongozi
kwamba, lazima wajiamini wao wenyewe. ‘’Wakijiamini wao wenyewe wanaweza kufikia malengo yao”
Pia ameshauri kwamba
ili tuweze kufikia lengo la hamsini kwa hamsini lazima vijana waanze
kukimbilia fursa mbali mbali katika jamii pindi zinapotokezea. Kujaribu kugombea
nafasi za uongozi na amesisitiza vijana kutambua kwamba "kupata na kukosa ni majaliwa lakini utakuwa ushajaribu".
WANANCHI WANAOMFAHAMU
Baadhi ya wananchi wanomfahamu Jamila wanasema, ni kijana
ambaye ametambua mapema uwezo wake wa kuongoza na anatumia uwezo huo kufikia
ndoto zake, na wanaamini atafika mbali sana.
Juma Bakari Juma
anasema "Jamila ni kiongozi kijana mwanamke na ni mlemavu wa macho lakini
anajituma sana na namini atakuwa kiongozi mzuri hapo baadae ametambuwa uwezo
wake wa kuongoza mapema".
Kwa upande wake Naila Mcha Haji anasema "Jamila ni mfano
kwa sisi vijana wa kike ambao hatuna
ulemavu wowote hapa mtaani kuna kitu cha
kujifunza maana Jamila anajituma kama anaona vile".
‘’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’mwisho’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’’
1 Comments
Mashallah mungu amzidishiye
ReplyDelete