Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake TAMWA-ZNZ Dkt,Mzuri Issa amesema ili tuweze kukuza usawa wa kijinsia visiwani Zanzibar kuna ulazima waandishi wa habari kutoa taarifa za wanawake na maendeleo yao katika Nyanja tofauti zikiwemo za uongozi, na maendeleo ya kijamii.
Amesema ili usawa wa kijinsia upatikae ni lazima kuwe na mkakati maalumu wa kuwajenga waandishi wa habari chipukizi ambao wataweza kutoa habari zinazohusus wanawake kwa ufanisi mkubwa.
Aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa siku moja wa kupitia mtaala maalumu utakaotumika kufundishia waandishi wa habari vijana kupitia mradi wa kuwajengea uwezo wanawake na uongozi kupitia vyombo vya habari.
‘’Kwa kuwa wanahabari ni sauti ya wasio na sauti, kuwa kupitia mafunzo hayo maalumu yatakayowajengea uwezo wanahabari vijana 18 kutoka Unguja na Pemba ninaamini kwamba watakwenda kutatua tatizo la muda mrefu lililokosa wakulisemea na kuwafanya wanawake wengi zaidi kushindwa kufikia malengo yao’’aliongezea.
Sambamba na hayo alisema pia mafunzo hayo yatawajenga wanahabari waweze kuandika habari zenye kuleta manufaa zaidi sambaba na kuwa wachambuzi wa mambo mbali mbali kupitia maandiko yao au vipindi watakayotaarisha wakati wakiendelea na mafunzo yao ya mwaka mmoja.
Awali akiwasilisha ripoti ya mtaala utakaotumika kuwafundishia wanahabari hao vijana Mhadhiri kutoka Chuo kikuu cha Taifa Zanzibar Dkt,Salum Sleiman Ali alisema wakati TAMWA-ZNZ inajipanga kufanya mafunzo kwa wanahabari hao vijana hawana budi kuzingatia yale yote yalio muhimu ambayo wanaamini yatawajengea uwezo wanahabari hao na kuwafanya kuwa wadadisi.
Akibainisha miongoni mwa vipengele muhimu ambavyo amependeleza kufundishwa ni pamoja na kuwajengea uwezo wanahabari hao vijana katika kutengeneza habari bora na zenye kuleta mabadiliko kwa jamii husika hususani kwa wanawake ambao ndio walengwa.
Baadhi ya wajumbe wakichangia ripoti hiyo walisema ni jambo jema kuwajengea uwezo wanahabari na walisema ni wajibu wa wale wote ambao watanufaika na mafunzo hayo kufanya kazi kwa bidii kuonesha uwezo wao wa kuisaidia jamii ya wanawake.
Mhadhiri kutoka Chuo kikuu cha Taifa Idara ya habari Imane Duwe alisema katika mafunzo hayo wanahabari wanapaswa pia kufundishwa namna bora ya kujitegemea na kujitolea zaidi kutokana na kuongezeka kwa wimbi kubwa la changamoto katika upatikanaji wa ajira.
Alisema wanahabari watakapofundishwa namna bora ya kuendesha kazi zao bila ya kuajiriwa wataweza kuibua mengi mazuri kwa faida ya jamii kwa kuwa hawatakua na sehemu ambayo watahofia kutoskilikana kwa kazi zao.
Nae msaidizi mhariri wa shirika la magazeti ya Serikali Zanzibar Juma Khamis alisema ili kujenga kizazi bora cha wanahabari watapaswa pia kufundishwa na kuzifahamu vyema kanuni za maadili ya uandishi wa habari kwa lengo la kuepuka kujingiza kwenye matatizo yanayoweza kuepukika.
Mradi wa kuwajengea uwezo wanahabari vijana 18 Zanzibar unatekelezwa na TAMWA-ZNZ kwa kushirikiana na shirika la The National Endowment for Democracy (NED) kutoka Marekani.
0 Comments