Na Gaspary Charles
Dkt. Mzuri Issa Ali. Daktari wa Falsafa katika Sayansi ya Jamii, mwanamke kinara aliyejitoa muda na maisha yake kupambana kutetea haki za wanawake na Watoto Tanzania na barani Afrika.
Awali Jamii Haikumuelewa, lakini sasa ulimwengu umemuelewa zaidi.
Safari na makuzi ya maisha yake kamwe haikuwa nyepesi. Ilikuwa ni safari yenye vikwazo na misukosuko chungu nzima, ikiwemo kukataliwa na kukatishwa tamaa juu ya ndoto zake alizokuwa nazo katika kuhakikisha anapambania uhuru na usawa wa haki kwa wanawake na watoto katika nyanja mbalimbali.
Na hii ni kutokana na mfumo dume uliokuwa umetawala miongoni mwa jamii alikokulia kwa kuamini kwamba mwanamke hawezi kusimama imara kupigania haki ya walio wengi.
Kamwe vikwazo hivyo havikuwahi kuwa kizuizi kwake kutimiza adhima yake, na badala yake, vilizidi kuchochea shauku ya kufikia lengo lake, na hapo ndipo safari yake ya ukombozi wa mwanamke na mtoto ikaanza.
Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Wanawake Ulimwenguni UN Women, mnamo March 04, 2021, kupitia tovuti yake lilichapisha chapisho maarufu lililobeba picha halisi ya Dkt. Mzuri Issa katika safari ya maisha yake.
‘This is what leadership looks like: Meet Mzuri Issa, breaking down social barriers to women’s leadership in Tanzania, using the media.
Ilikuwa ndicho kichwa habari katika andika hilo kubwa na refu, kikiwa na maana kwamba,
Hivi ndivyo uongozi unavyoonekana: Kutana na Mzuri Issa, akivunja vikwazo vya kijamii kwa uongozi wa wanawake Tanzania, kwa kutumia vyombo vya habari.
Katika chapisho hilo, Dkt. Mzuri ananukuliwa kukiri kuwahi kukataliwa katika historia ya safari ya makuzi yake kutokana na ugumu wa maisha ya familia yake iliyokuwa ikikabiliana nayo hasa mama yake.
“Mama yangu hakuwa na uwezo wa kunilea, na nilitumia muda mwingi wa utoto wangu nikihama kutoka nyumba moja hadi nyingine,” alieleza Dkt. Mzuri.
Mnamo February 1998, safari yake ya uandishi wa habari ndipo ilianza rasmi akifanyia kazi katika Gazeti maarufu na lakipekee visiwani Zanzibar kwa wakati huo gazeti la NURU ambalo baadae lilibadilishwa jina na sasa likifahamika kama gaeti la Zanzibar leo.
Katika chapisho hilo anasema alipata mafunzo muhimu kuhusu maisha kutokana na mazingira yaliyomzunguka, mazingira ambayo yalimsukuma kumaliza elimu yake na ndipo alichagua kazi ya uandishi wa habari kwa lengo moja tu, kutetea na kupigania haki za wanawake na watoto na ndipo akashiriki kuanzisha Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania TAMWA tawi la Zanzibar mwaka 2004, akitekeleza majukumu yake hapo kwa umahiri mkubwa.
Alieleza, "nilikua mtu mzima haraka sana. Nikiwa na umri wa miaka 11, nilikuwa nikifanya kazi kwenye kioski cha vyakula vya haraka ili tu nipate chakula kila siku. Nilishuhudia aina nyingi za ubaguzi na unyanyasaji dhidi ya wanawake na watoto, akiwemo mama yangu mwenyewe.”
Umahiri na ndoto zake za kuifanya dunia kuwa sehemu salama kwa wananwake na Watoto zilizidi kuleta tija kwa jamii ya walio wengi akiwa chini ya TAMWA kama mratibu wa shughuli za chama hicho visiwani Zanzibar, kabla ya mwaka 2017 kukabidhiwa rasmi kijiti kuwa mkurugenzi wa chama hicho nafasi ambayo anaihudumu mpaka wakati huu.
Akifanya kazi na TAMWA Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa Ali, amefanikiwa pakubwa kurejesha matumaini ya wanawake na Watoto walio wengi kuondokana na kadhia mbaya dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia ambayo umewaathiri wanajamii walio wengi visiwani humu.
Ambapo mwaka 2021 TAMWA Zanzibar imechaguliwa kuwa miongoni mwa mashirika 6 yaliyotambuliwa na shirika la UN Women na mashirika ya wanawake kuwa miongoni mwa taasisi zilizo msitari wambele katika kupambana na udhalilishaji.
Na mwaka 2020 Dkt. Mzuri Isa Ali alitunukiwa tuzo ya Zanzibar Youth award kwa mchango na mafanikio yake katika kupambana kumuinua mwanamke wa Zanzibar.
Huyo ndie Dkt. Mzuri Issa Ali, aliyepata kuhudumu nafasi ya kaimu mkurugenzi, Kurugenzi ya Mawasiliano Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na Msaidizi Katibu wa Habari wa Rais wa Zanzibar kwa nyakati tofauti.
Ambaye safari ya maisha yake imeongeza kasi kuvunjwa kwa minyororo ya dhana potofu na mfumo dume dhidi ya wanawake visiwani Zanzibar, na kufungua milango zaidi kwa wanawake wengi kupata ujasiri na uthubutu wa kusimama kudai haki zao katika nyanja mbalimbali ikiwemo masuala ya ungozi na vita dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na Watoto.
Yapo mengi ya kusimulia kuhusu kuhusu safari ya ukombozi wa haki za wanawake na Watoto Zanzibar ya Dkt. Mzuri Issa Ali, aliyezaliwa mnamo January 13, 1976. Lakini kwa leo naishia hapa kwa kusimulia machache kati ya mengi juu yake.
1 Comments
UGA MEDIA I Furaha Yako
ReplyDelete