Mkurugenzi wa TAMWA Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa akizungumza na wanakikundi cha Muungano kilichopo Sehia ya Makngale Wilaya ya Micheqeni wakati wa ziara ya kutembelea kikundi hicho. |
Mwani uliozalishwa na wanakikundi ukiwa umefifadhiwa ndani kusubiri wateja. |
Na Gaspary Charles- TAMWA ZNZ
WAKULIMA wa mwani kisiwani Pemba
wameiomba serikali ya mapinduzi ya Zanzibar kuingilia kati upatikanaji wa soko
la zao hilo ili kuwanusuru na hali ngumu ya maisha wanayokabiliana nayo
kutokana na wanunuzi kusitisha ununuaji zao hilo.
Hayo yamebainishwa na wanakikindi
cha Muungano kilichopo Shehia ya Makangale Wilaya ya Micheweni mkoa wa
Kaskazini Pemba wakati wakizungumza na mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa
Habari Wanawake Tanzania, TAMWA Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa alipowatembelea
kukagua maendeleo ya kikudi hicho.
Haji Hamad Haji mmoja wa
wanakikundi hicho amesema licha ya wananchi wengi Zanzibar kuhamasika kuzalisha
kwa wingi zao hilo lakini kukosekana kwa soko inazidi kudumaza hali za wakulima
hao bila kujua nini cha kufanya zaidi.
“Ukija vijijini watu tunateseka
sana na zao hili, migongo imevunjika kwa kuzalisha mwani lakini manufaa hapana.
Saizi tumevuna lakini tumebaki kuuweka ndani kutokana na hatuna wa kumuuzia,”
alisema
Aidha alisema tatizo hilo
linatokana na wananchi kukosa taaluma zaidi ya namna ya kusarifu mwani kwa
matumizi mengine jambo ambalo linapelekea wakulima wengi kutegemea njia moja ya
uuzaji bila kuwa na mbadala wake.
Alisema, “wakulima tunakumbana na
shida hii kutokana na kwamba bado tunakosa taaluma ya kusarifu mwani. Kila siku
tunaambiwa mwani unamatumizi mengi lakini sisi wakulima hatuijui taaluma hiyo
na hivyo kupelekea kutegemea soko eneo moja kwa kampuni za mwani na matokeo
yake ni haya wamesitisha kununua na mwani tumesalia nao majumbani.”
Kwa upande wake Time Ismail Ali mwenyekiti
wa kikundi hicho, alisema tangu wanunuzi wasitishe kununua zao hilo ambalo kwa
kiwango kikubwa linazalishwa na wanawake imepelekea familia nyingi kukumbwa na hali
ngumu ya maisha.
“Kusema ukweli soko la mwani
limetuathiri sana wakulima hapa Makangale hasa sisi wanawake kwani wanawake
wengi hiki ndicho kilimo chetu na tulikuwa tukipata angalau pesa kidogo ya
kujikimu na familia zetu lakini hali imekuwa tofauti tangu makampuni yasitishe
kununua mwani. Tunavuna sana lakini upo ndani unaoza hatuna pa kupeleka,”
alisema.
Aidha aliongeza kutokana na
tatizo hilo imepelekea wakulima wengi kukata tamaa ya kuendelea na uzalishaji
wake jambo ambalo linazidi kuhatarisha uchumi wa familia hizo.
“Angalia chumba hiki chote
kimejaa mwani, tumevuna lakini umekuwa wa kutunza ndani kutokana na hakuna
mteja wa kumuuzia,” alisema Time huku akionesha chumba ambacho amehifadhia
mwani wake.
Kutokana na hilo aliiomba
serikali kusaidia kumaliza tatizo hilo kwani hali kuendelea kuwa hivyo
inahatarisha kutokea madhara zaidi kwa wananchi wanaotegemea zao hilo ikiwa ni
pamoja na tatizo la njaa kwani wakulima wengi hutegemea kuuza mwani ili wapate
pesa za kununulia chakula kwenye familia.
“Tunaiomba sana serikali kama
ilivyofanya kwenye Karafuu basi ituangalie nasisi wakulima wa Mwani kwani hali
ni mbaya kwa sasa.Tunatumia nguvu nyingi kuzalisha lakini ikifika wakati wa
kuuza wateja hakuna kama ambavyo ilivyo sasa na hata mteja akipatikana bei yake
bado ni ndogo sana kulingana na gharama za uzalishaji wake,”alisema.
Aliongeza, “bei ya mwani kwasasa ni
shilingi 600 sasa embu jifikirie mkulima utauza kilo ngapi ili upate pesa za
kutosha kununulia chakula cha familia?”
Kwa upande wake Khadija Masoud
Ali alisema licha ya kukabiliana na changamoto hizo lakini pia ukosefu wa zana
bora za kuwawezesha kuzalisha ni kikwazo kwao jambo ambalo linapelekea
kukumbana na viumbe hatarishi wanaotishia usalama wao wawapo baharini.
“Sisi wakulima bado tunafanya
kazi katika mazingira magumu sana kwani hatuna zana bora za kujilinda
tunapokuwa baharini. Wakati mwingine tunang’atwa na wadudu hatarishi na
kusababisha kukaa ndani miezi zaidi ya mitatu na wengine kupata ulemavu wa
kudumu,” alisema mwanakikundi huyo.
Mapema mkurugenzi wa TAMWA
Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa aliwataka wakulima hao kutokata tamaa na uzalishaji
ili kujiendeleza kichumi licha ya changamoto zinazowakabili.
“Kikubwa tuendelee na uzalishaji
tusirudi nyuma kwani ndiyo shughuli zetu. Nasisi wadau tutajitahidi kuwasilisha
changamoto zenu sehemu husika ili angalau ziweze kutafutiwa ufumbuzi na kilimo
hiki kiweze kuwa mkombozi kwa wakulima kama mazao mengine yanayolimwa hapa
Zanzibar,” alisema Mkurugenzi.
Ziara ya Mkurugenzi wa TAMWA
Zanzibar, Dkt. Mzuri Issa kisiwani Pemba ililenga kutembelea na kugagua
maendeleo ya vikundi vya wanawake wajasiriamali vinavyowezeshwa na TAMWA ZNZ
kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake Kiuchumi Zanzibar WEZA unatotekelezwa
Zanzibar na TAMWA ZNZ kwa ufadhili wa taasisi ya Zanzibar Milele Foundation.
0 Comments