HABARI MPYA

6/recent/ticker-posts

MFAHAMU (HALLA) ALIYEWACHOCHEA WANAWAKE WENGI KUFANYA BIASHARA ZA MITANDAONI ZANZIBAR.


 Safari inaanzia Maeneo ya Amani hadi katika mtaa wa Mikunguni mtaa ambao ndani yake kuna Hospitali maarufu kwa macho kwa hapa Zanzibar, lakini safari yetu inaishia nyuma ya Hospitali hiyo Nyumbani kwa Haitham Mohd Baraka maarufu HALLA Mwanaharakati na Mjasiriamali wa bidhaa mbalimbali za mitandaoni hapa visiwani Zanzibar.

Ki kawaida Halla ni mtu ambaye hubanwa sana na matumizi ya simu kwa kuongea na hata kwa njia ya kutuma ujumbe mfupi na sauti kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii kwa kuongea na wateja wake.

Na hali hii ilianza muda mrefu tokea alipogundua fursa ya kibiashara wakati alipokuwa Dubai na familia yake, ingawa jambo hili lilimsbabishia changamoto kubwa kwenye maisha yake lakini alijaribu kuzishinda na kusimama hadi sasa amekuwa mwanammke wa pekee na mwenye kuaminika na wengi visiwani hapa kwa biashara hiyo.

Haitham (Halla) mara baada ya kugundua kuwa kwenye ofisi nyingi kuna shida ya upatikanaji wa vyakula miongoni mwa hizo ni hile aliyokuwa akifanya kazi mwenza wake, jambo lililomfanya aanze biashara ya uuzaji wa vyakula katika ofisi mbalimbali nchini Dubai, jambo ambalo lilimkasirisha sana mwenza wake na kumkataza kufanya kazi hiyo.

Geuza changamoto kuwa Fursa ni kauli maarufu ambayo hutumiwa na watu wengi katika kumshajihisha mtu ama jamii ya watu flani kujihangaikia katika kujitafutia kipato bila ya kujali magumu wanayopitia, japokuwa wengi hushindwa lakini kwa Halla licha ya makatazo mengi hakusita kufanya kazi hiyo kwani ilikuwa ikimuingizia kipato kilichomuwezesha kujikimu kimaisha na kutanua wigo wa kuanzisha biashara ya mitandaoni na kuanza kusafirisha bidhaa mbalimbali kutoka Dubai hadi Zanzibar.

Titi Mohammed ni mwanammke mashuhuri na aliyekuwa mstari wa mbele wakati wa kutafutafua uhuru wa Tanganyika, mara baada ya kupatikanwa uhuru wa Tanganyika na kuundwa baraza la mawaziri la kwanza la Tanganyika Bibi Titi alikerwa na hali ya kutoaminika kwa wanawake na katika serikali hiyo, hii inakwenda sambamba na wafanyabiashra za mitandaoni kwa kutoaminiwa na wateja wao japokuwa kwa Hala imekuwa ni tofauti kwani uaminifu kwa wateja hasa kwa kutumia muda mdogo kwa bidhaa zinazoagiziwa na wateja wake jambo ambalo wengi wamekuwa wakimsifu kwa uaminifu huo.

Nikirejea maneno ya mama mzazi wa Haitham alikuwa akitarajia mwanawe huyo kufanya kazi ya uhudumu wa ndege jambo lililoshindikana kwake na kurithi biashara aliyokuwa akiifanya mama yake kwa wakati wote, hata hivyo mama wa Haitham alisema kuwa anafurahishwa na hali hiyo ya mwanawe kwani amekuwa akifany kitu anachokipenda.

Nikimnukuu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mh Omar Said Shaaban wakati akiwasilisha Hotuba katika Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 akautaja mpango wa Serikali wa kuanzisha mradi wa KHALIFA FUND wenye lengo la kuwasaidia wajasiriamali wadogo wadogo, wadogo na wa kati katika kujikwamua kiuchumi kwa kuwapatia mikopo yenye gharama nafuu, mafunzo ya ujasiriamali pamoja na uboreshaji wa bidhaa wanazozizalisha ili ziweze kuongeza ushindani katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Mradi huo ulipangiwa jumla ya Shilingi bilioni 9.1, kati ya fedha hizo Shilingi bilioni 4.5 kutoka Serikalini na Shilingi bilioni 4.6 kutoka kwenye mfuko wa Khalifa Fund.

Mkuu wa Wilaya ya Magharibi B Hamida Mussa Khamisi akiwa ni mmoja miongoni mwa wateja wa HALLA anaeleza kuwa uwezo na ubora aliokuwa nao hasa katika kusimamia biashara yake umeafanya wanawake hasa wa wilaya yake kuwa wajasiriamali wakub wa wa bidhaa mbalimbali ambazo huzipata kwa Haitham.

Aidha alieleza kuwa kwa upande wa serikali wanaendelea kuwajengea mazingira bora wajasiriamali kwa kuwapatia maeneo stahiki na mikopo nafuu itakayowasaidia kueleza kukuza biashara zao.

Baadhi ya wajasiriamali na wafanyabiashara waliofanikiwa kibiashara na wengine hata kuanzisha bishara zao wenyewe walielezea kuridhika kwao na namna ambavyo muda wote wamekuwa na Halla kibiashara na nmna ambavyo amekuwa kinara katika kusimamia biashara zao kukuwa kila siku.

Baada ya ushuhuda huo nimalizie kwa kusema tu kuna fursa nyingi hivi sasa kwa wajasiriamali wa sekta tofauti ikizingatiwa Serikali imechukua dhamana ya kuvipatia mikopo vikundi hivyo ili kupunguza ukali wa maisha kwa wananchi wake, hivyo ni wakati wa kuchangamkia fursa hiyo hasa wanawake na Akinamama, usijidogoshe wala kujidumaza na kusema kuwa hutaweza jenga uthubutu simama kwani kila kitu kinahitaji uthubhutu, utayari na kujiamini.

 

Post a Comment

0 Comments