Na Essau kalukubila.
WANAWAKE wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi wametakiwa
kuelewa mbinu sahihi za kufanya ushawishi katika siasa na uongozi ili kukabiliana
na vikwazo vinavyoweza kuwakwaza kushika nafasi hizo katika ngazi mbalimbali.
Wito huo umetolewa na mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Taifa
Zanzibar -SUZA, Dkt. Salum Suleiman Ali, wakati wa mafunzo maalum kwa wanawake
kutoka vyamba mbalimbali vya siasa Pemba kuwajengea uwezo kutambua haki zao na
kushiriki katika mchakato wa kugombea nafasi za uongozi kwenye vyombo vya
maamuzi.
Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Chama cha
Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania, Zanzibar (TAMWA ZNZ) kwa kushirikiana na
Ubalozi wa Norway alieleza suala la kushiriki kugombea nafasi za uongozi ni
mchakato endelevu unaohitaji maadalizi ya muda mrefu ili kujenga Imani kwa
jamii juu ya uwezo wa kiongozi katika kutetea na kusimamia changamoto zao.
Alifahamisha ili wanawake waweze kufanikiwa kushika nafasi za
kisiasa na uongozi katika ngazi mbalimbali uwezo wa kujenga hoja na kuibua
changamoto zinazowakabili wananchi ni mbinu muhimu katika kuongeza ushawishi
wao kwa jamii.
Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025, Dkt. Salum aliwahimiza
wanawake kuanza kutumia fursa ya vyombo vya habari kuweka ajenda ya kuisemea
jamii matatizo yao ili kusaidia kupata suluhisho.
“Lazima tuvitumie vyombo vya habari kwaajili ya kufanya
ushawishi wa mabadiliko kwa kutengeneza ujumbe na maudhui yanayolenga kuwasemea
wananchi matatizo yanayowakabili hii itatusaidia kujijenga kisiasa na kuaminika
kwa umma kuliko kusubiri uchaguzi umefika ndipo tuanze kujitokeza kutaka
kuwasemea wananchi,” alifahamisha mkufunzi huyo.
Aliongeza TAMWA Zanzibar kwa kushirikiana na Ubalozi wa
Norway kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake katika masuala ya uongozi (SWIL) imechapisha
muongozo maalum ambao unatoa mwelekeo kwa wanawake kutambua mbinu za kutumia
kushinda nafasi za uongozi katika ngazi mbalimbali.
Alieleza, “TAMWA ZNZ imeandaa kitini maalum kwaajili ya kutoa
muongozo kwa wanawake wagombea watarajiwa kujijengea uwezo wa kushiriki katika
mchakato wa kugombea nafasi za kisiasa na uongozi pamoja na michakato yote ya
kidemokrasia.”
Mapema mratibu wa TAMWA ZNZ, Fat-hiya Mussa Said alieleza
mafunzo yamewashirikisha wanawake kutoka vyama mbalimbali vya siasa pamoja na
viongozi wa serikali za wanafunzi wa vyuo vikuu na vya kati kwaajili ya
kuwaunganisha na kubadilishana uzoefu kuelekea kugombea nafasi mabilmbali za
uongozi.
Aliongeza kuwa mafunzo hayo yanatolewa kwa wanawake kwaajili
ya kuwajengea ujasiri na uthubutu wa kuwa tayari kushiriki kugombea na kudai
haki za wanawake katika nafasi mbalimbali za uongozi
Alieleza, “mafunzo haya yanalenga kuwawezesha wanawake kuwa
na ujasiri na uwezo wa kusimama kutetea haki za msingi za wanawake kwenye
masuala ya uongozi ikiwa ni pamoja na kuwa tayari kugombea uongozi kwenye chaguzi
mbalimbali za kidemokrasia.”
Kwa upande wake Saghira Moh’d Khalfan mmoja wa washiriki hao alishukuru
TAMWA ZNZ kwa kuandaa muongozo huo maalum kwaajili ya kuwaonesha njia wanawake
kushiriki katika nafasi za uongozi kwani utawasaidia kwenye uchaguzi mkuu 2025 kukabiliana
na changamoto zilizokuwa zikiwakatisha kufikia malengo yao kwenye uongozi.
TAMWA Zanzibar kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake kushiriki katika uongozi SWILPROJECT unaotekelezwa kwa mashirikiano na Ubalozi wa Norway inasaidia kufanikisha utekelezaji wa Lengo namba Tano la Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa linalohimiza kuwepo kwa Usawa wa Kijinsia kwa Wanawake na wasichana.
0 Comments