ZAIDI ya wananchi 561 wamefikiwa na wahamaishaji jamii Kisiwani Pemba, kati yao wanawake wakiwa 384 na wanaume 177 kutoka shehia mbali mbali, kupitia mikutano ya ufuatiliaji iliyofanywa na wahamasihaji hao.
Hayo yamebainika wakati wa uwasilishaji wa ripoti za wahamasiahji hao, kipindi cha Septemba hadi Febuari mwaka huu, mkutano uliofanyika mjini Chake Chake, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa kuwawezesha wanawake katika nafasi za uongozi(SWIL) unaotekelezwa kwa maishirikiano na TAMWA Zanzibar, PEGAO na ZAFELA kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway.
Wahamaishaji hao wamesema wananchi hao waliweza kuwafikia kupitia mikutano waliokuwa wakiifanya katika shehia hizo, huku wengi wao wakiwa ni wanawake na tayari baadhi yao wameonesha nia ya kuingia majimboni kuwania nafasi za uongozi katika uchaguzi mkuu 2025.
Wamesema kwa sasa wanawake wamehamaisika zaidi kufuatia elimu mbali mbali inayotolewa, huku baadhi ya wanaume nao tayari wameshanza kuelewa malengo ya wahamaishaji hao.
Mmoja wa wahamaishaji hao kutoka Wilaya ya Chake Chake, Ali Abdalla, alisema katika shehia walizozifikia waliweza kuibua wanawake wenye nia ya kuwania nafasi za uongozi, na kuendelea kuhamasisha jamii juu ya uongozi kwa wanawake.
“Pia tumebaini kuwa wanawake wenyewe hawapendani, huku baadhi ya wanaume hawako tayari kuona wanawake wanaingia katika uongozi, lakini tunaendelea kuwapatia elimu ili kufahamu dhana nzima na mwisho wa siku wanawanaruhusu,”alisema.
Akizungumzia Changamoto katika shehia ya Mfikiwa na Wawi, alisema wamebaini ajira za watoto muda wa kwenda skuli huuza korosho, upangishaji holela kwa wageni wanaotaka Tanzania bara na kwenda kinyume na maadili ya maeneo wanayofikia.
Naye mhamaishaji jamii kutoka Wilaya ya Micheweni Mariyam Hemed Said, alisema waliweza kuwafikia wananchi katika Shehia ya kiuyu mbuyuni, Shanake na Maziwa Ng’ombe na kuutambulisha mradi wa SWIL na kujua changamoto zinazowakabili katika shehia zao.
Alisema changamoto kubwa iliyoibuliwa ni ubovu wa barabara, uhaba wa madaktari na vifaa tiba katika kituo chao cha afya, bei ndogo ya zao la mwani, uhaba wa walimu skuli, pamoja na utoro wa wanafunzi skuli kwa kujiingiza katika uokotaji wa koya la baharini.
“Wapo baadhi ya wanawake walitufuata baada ya kuwapatia elimu na kuonesha nia ya kutaka kuwania nafasi za uongozi majimboni,”alisema.
Akifungua mkutano huo Mkurugenzi Mradi wa SWIL kutoka PEGAO Hafidh Abdi Said, alisema mwisho wa siku wanataka kuona mafanikio ya mradi ili ikifika 2025 kuwe na matokeo makubwa kwa wanawake kujiotokeza kwa wingi kuingia majimboni kuwania nafasi za uongozi.
Alisema asilimia 75 ya matokeo ya mradi yanategemewa kutoka Pemba, hivyo PEGAO inahitaji kuona matokeo na kitu cha maana kilichofanyika, huku wakitambua mradi wa SWIL unategemea zaidi wahamasiahji jamii kufika katika jamii na kuwawezesha uwezo kudai haki zao za msingi.
“Tuhakikishe watu wanaotaka kutia nia wanapaswa kufuatiliwa na mwisho wa siku tupate watu wazuri na wenye nia nzuri sio kila mtu atakaegombania atapata nafasi, nia yetu mradi ifikie angalia 50%,”alisema mkurugenzi.
Mapema mratibu wa mradi mradi wa kuwawezesha wanawake katika nafasi za uongozi (SWIL), Dina Juma alisema malengo ya mradi ni kumsaidia mwanamke na kuijengea uwezo jamii kubaini changamoto zinazowakabili na kudai haki zao ili waweze kuingia katika nafasi za uongozi.
Naye Mwakilishi kutoka TAMWA Pemba Asha Mussa Omar, aliwataka wahamaishaji jamii hao kuhakikisha ripoti zao wanazoziwasilisha zinaziba mapengo yote yaliyojitokeza katika ripoti zilizopita ili kufikia lengo la kuidaidia jamii kuondokana na changamoto.
Mradi wa ushirikishwaji wanawake katika uongozi na demokrasia unatekelezwa kwa mashirikiano na TAMWA Zanzibar, PEGAO na ZAFELA kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway.
0 Comments