HABARI MPYA

6/recent/ticker-posts

Mbakaji Zanzibar aokolewa na Polisi kwa Mabomu


 

Jeshi la Polisi Zanzibar limelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliokua na hasira waliotaka kumshambulia kijana mmoja anaedaiwa kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 10.

Tukio hilo limetokea majira ya saa tatu asubuhi wakati mtuhumiwa huyo alipohifadhiwa katika nyumba ya sheha wa shehia ya Kisauni nje kidogo na Mji wa Zanzibar.

Awali wananchi waliokua na hasira walitaka kumpiga na wakitishia kumuua kijana huyo ambae amepigwa na kuumizwa vibaya baada ya kushuhudiwa akimfanyia kitendo cha ubakaji mtoto huyo ambae jina limehifadhiwa.

Baadhi ya waandishi wa habari walishuhudia kundi kubwa la watu wakiwa nje ya nyumba ya Sheha wa Shehia hiyo huku taratibu za kumkinga na kumhami mtuhumiwa huyo ili asidhuriwe na watu hao zikifanyika ambapo tayari alishachezea kipigo cha wananchi hao.

“Wananchi walikuwa na hasira sana kutokana na vitendo hivi ambavyo vinatokea kila siku na kuendelea kuwadhalilisha watoto na ndio maana wananchi wamechoshwa, na kama sio jeshi la polisi yule kijana angeuliwa kabisa kutokana na hasira za watu” alisema shuhuda mmoja alitekuwa nje ya nyumba ya Sheha.

wananchi hao wameviomba vyombo vya sheia kuhakikisha wanatoa adhabu kali kwa mujibu wa sheria  kwa watuhumiwa wa vitendo vya udhalilishaji , pamoja na kuwadhiditi kuhakikisha kwamba hawatoroki  na wanatumikia adhabu zao wanazohukumiwa.

Awali wananchi hao walikusanyika nje ya nyumba ya Sheha wakitaka mtuhumiwa huyo atolewe waachiwe wampige huku wakijaribu kutaka kuvunja milango ambapo tayari Sheha akiwa ameshatoa taarifa polisi ili mtuhumiwa kuja kuchukuliwa na kupelekwa katika vyombo vya sheria.

Hafla askari wachache walifika katika tukio hilo lakini walizidiwa nguvu na wananchi waliokuwa na hasira kali na kuongeza nguvu ya kuita askari wengine ambapo walipofika walilazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao katika eneo hilo.

Sheha wa Kisauni Hija Suleiman, alisema kuwa mtuhumiwa huyo alifikishwa kwake baada ya kukutwa akimfanyia kitendo cha udhalilishaji mtoto huyo ambae ni mwanafunzi wa shule ya msingi.

"Wananchi walikua na hasira kali sana kama nisingemfungia ndani mwangu katika nyumba yangu wangemuua"alisema huku akitikisa kichwa kuonesha hali haikuwa ya kawaida.

Sheha Suleiman alisema mtoto huyo aliyefanyiwa udhalilishaji ni mkaazi wa shehia yake ya lakini mtuhumiwa sio mkaazi wa shehia yake.

Mundhir Ali Bakar ni shuhuda ambae alimkuta mtuhumiwa anafanyiwa kitendo cha udhalikishaji alisema, alimkuta mtuhumiwa katika jumba bovu eneo la Kisauni Kidutani akimfanyiwa kitendo hicho na alipoona kuwa ameshafumwa mtuhumiwa akakimbia mbio.

Alisema alipambana nae kufukuza na hatimae akamkamata na kuomba msaada kwa watu wengine ambao walifika katika eneo hilo kuja kumsaidia kijana huyo.

"Wakati napita eneo la tukio nilimsikia mtoto analia anapiga kelele sana sauti iliyoashiria anafanyiwa kitu kibaya katika jumba bovu na nilipoangalia nikamkuta tayari ameshamvua nguo anamfanyia kitendo cha udhalilishaji huku akiwa amemuwekea kisu shingoni" alisema Shuhuda huyo.

Aidha Shuhuda huyo alisema mtuhumiwa huyo wakati anapambana nae katika harakati za kujinasua alitoa kisu na kumpiga nacho mkononi lakini wakifanikiwa kumkamata na kumpeleka kwa Sheha kwa hatua nyengine zaidi.

Akielezea kilichomtokea Mtoto huyo alisema aliefanyiwa kitendo hicho, alisema alitoka kwao anaelekea Madrasa na alipokuwa njiani alitokea mtu huyo akiwa amepanda bodaboda na kumuambia apande katika bodaboda amuwahishe Madrassa ili asichelewe.

"Kasimamisha bodaboda yake akanambia panda nikupeleke, nikapanda, nilipofika eneo la Madrasa nilimuambia kuwa nimeshafika lakini alikataa kunishusha nikaaza kupiga kelele lakini alipeleka mbio bodaboda nakunipeleka katika lile jumba na kanambia nikipiga kelele ataniua "alisema Mtoto huyo huku akilia.

Mtuhumiwa wa tukio hilo Idrisa Juma Pandu alikiri kufanya tukio hilo na kusema kuwa haikuwa akili yake kwa kudai alikuwa naafanya jambo hilo bila ya kutegemea.

Akizungumzia tukio hilo kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, Awadhi Juma, alisema kuwa mtuhumiwa huyo yupo kituo cha polisi Mazizini wanamshikilia kwa hatua za kisheria.

Alisema mtuhumiwa huyo anakabiliwa na malalamiko matatu ambayo yameripotiwa kituoni hapo hiyo jana ambapo yaliibuka baada ya wananchi kusikia amekamatwa mtu kwa kosa la ubakaji na ndipo wengine wakenda kushuhudia mtu huyo na ndipo walipombaini kuwa nyie yeye.

Kamanda Awadh aliwaambia waandishi wa habari kwamba matukio yote hayo ya uhalifu ameyafanya kijana huyo kwa siku moja kwa nyakati tofauti na maeneo tofauti.

Alisema kabla ya kufanya ubakaji, majira ya saa 12 asubuhi kijana huyo alimpora mama mmoja mkoba wake ukiwa na simu na fedha, baadae  majira ya saa moja asubuhi alitaka kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka 14 eneo la Mombasa Mbuyumnene lakini mtoto huyo alifanikiwa kukimbia kwao mbio.
“Huyu kijana anaonesha amekusudia kweli kwa sababu kuna mtoto hapa amempakia halafu yule mtoto akapiga kelele na akchupa kwenye bodaboda yake inaonesha alikuwa anataka kutenda kitendo kiovu maana huyu mtoto anasema kila akimwambia nishushe ndio anazidisha mwendo lakini Mungu akamjaalia akashupa akaanguka chini na kukimbilia kwao” alisema jirani mmoja wa Mombasa.

Alisema baada ya kumkosa mtoto huyo ndipo alipokwenda kumdhalilisha mtoto wa miaka 10 eneo la Kisauni na kuonekana na kijana mmoja ambaye alipambana naye na kisha kufanikiwa kuwaita watu waje kumsaidia kabla ya kupelekwa kwa Sheha.

Kamanda Awadh alikiri kuwa jeshi la polisi lililazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi waliokua na hasira kali kutaka kumshambulia mtuhumiwa huyo kutokana na kutaka kumuokoa kijana huyo asije kudhuriwa.

Alisema ni kweli vitendo hivyo vinaumiza lakini amewataka wananchi kutochukua sheria mikononi mwao kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria na huenda wakajikuta nao wanafanya makosa makubwa.

Mohammed Mahmoud Hassan ni muweka hazina mkuu wa jumuiya ya bodaboda Zanzibar amewataka wananchi kuchukua tahadhari kwa wanaotaka kupanda bodaboda kuhakikisha wanachukua namba ya simu, na kuchukua namba za vikoti wanavyovaa ili inapotokea jambo lolote waweze kuripoti namba hizo ili watafutwe.
“Nawashauri wanaotaka kupanda bodaboda wachukue tahadhari namba za simu na namba ya kikoti anachovaa dereva wa bodaboda kwa sababu unapochukua namba yake anapofanya jambo lolote la kihalifu ataweza kupatikana kwa kutokana na namba hizo, ni muhimu sana” alisema Hassan. 

Aidha aliiomba jamii kutowadhania dhana mbaya madereva wote wa bodaboda  na badala yake wale tu wanaofanya vitendo hivyo viovu ndio wanaotaka kuwaharibia wenziwao, hivyo ameliomba jeshi la polisi wawachukuliwe hatua za kisheria ili iwe funzo kwa wengine wenye tabia kama hizo za udhalilishaji.

Wakati hayo yakijiri Mkurugenzi wa Chama cha waandishi wa habari Wanawake TAMWA-ZNZ Dkt Mzuri Issa amewashauri wazazi na walezi  kuhakikisha wanafuatilia vyema nyendo za watoto wao wakati wanapokuwa nje ya nyumba zao ili kuepukana na vitendo kama hivyo vya udhalilishaji.

“Tunawashauri wazazi na walezi kujitahidi kuwaangalia watoto wanapotoka nje ya nyumba zao kwa mfano watoto wapokwenda skuli au madrassa basi wahakikishe wanawaambatanisha na watu waaminifu mpaka wanafika au kufuatilia na wasimuachie mtoto peke yake kwani hawajui yanayotokea njiani huenda akakutwa na kitu kibaya mzee hana habari” alisema Dk Mzuri.

Dk Mzuri alisema suala la ulezi wa watoto halipaswi kuzingatiwa zaidi watoto wanapokua nyumbani tu bali hata sehemu wanazokwenda ikiwemo maeneo wanayocheza, wanayosoma na maeneo yote yalio nje ya nyumba zao.

Post a Comment

0 Comments