Siku
moja baada ya kuachiwa kwa dhamana viongozi wake, Chadema imetaka
jumuiya ya kimataifa kuacha kuifadhili Tanzania, ikidai kuna ukiukwaji
wa demokrasia na haki za binadamu.
Tamko
hilo lilitolewa na mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alipozungumza na
waandishi wa habari jana kuhusu kuendelea kukamatwa kwa viongozi wa
chama hicho, akiwemo Dk Vicent Mashinji, ambaye ni katibu mkuu
aliyekamatwa Jumamosi akiwa Mbambabay wilayani Nyasa.
Wengine
waliokamatwa ni Cecil Mwambe, ambaye ni mwenyekiti wa Kanda ya Kusini
na mbunge wa Ndanda, Philbert Ngatunga (katibu wa kanda) na Manawa
Samuda (ofisa wa operesheni na mafunzo).
Pamoja
nao ni Zubeda Sakuru (mbunge wa viti maalum, Ruvuma), Asia Mohamed
(ofisa wa kanda), Ireneus Ngwatura (mwenyekiti wa Mkoa wa Ruvuma),
Delphin Ngaiza (katibu wa Mkoa wa Ruvuma), Cuthbert Ngwata (mwenyekiti
wa Wilaya ya Nyasa) na Charles Makunguru (katibu wa uenezi wa Wilaya ya
Nyasa).
Ilikuwa
ni siku chache baada ya viongozi na wanachama 51 kukamatwa Julai 8
wakiwa kwenye kikao cha ndani wilayani Chato mkoani Geita.
Vitendo hivyo viliifanya Chadema itoe tamko zito jana.
“Nchi zinazoupa fedha uongozi wa Rais (John) Magufuli, hazina budi kuacha,” alisema Lissu akitoa mfano wa jinsi Afrika Kusini ilivyotengwa wakati wa siasa za ubaguzi.
“Hawatakiwi kupewa fedha ambazo zitakandamiza Watanzania, ambazo zitauza demokrasia.”
Lissu, ambaye anajulikana kwa kutumia maneno mazito, alito mifano mingi aliyodai inaonyesha kukandamizwa kwa demokrasia.
“Wao wanafanya mikutano ambayo sisi tumezuiwa, wanafanya mikutano ya ndani ambayo sisi tumezuiwa,” alisema Lissu, ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki.
Lissu
alisema sasa ni wakati wa kuacha woga na badala yake kupaza sauti
kimataifa kupinga, kile alichoita ni ukandamizaji wa demokrasia ili
wahisani wainyime misaada Serikali ya Tanzania.
Mwanasheria
huyo alihoji kitendo cha majaji wa Mahakama Kuu kujiuzulu bila
kujulikana sababu licha ya baadhi yao kuhusishwa na sakata la uchotwaji
fedha kutoka Akaunti ya Tegeta Escrow iliyokuwa Benki Kuu (BoT).
Lissu
pia alizungumzia matumizi ya Jeshi la Polisi akishauri lisiendelee
kutumika kukamata wanasiasa wa upinzani ambao wanafanya mikutano na
vikao vya ndani kwa kuzingatia sheria na Katiba, badala yake litumike
kukamata wahalifu.
“Kila Polisi aliyenikamata anasema ‘bwana we tumeagizwa kutoka juu’. Sasa hili ni jeshi la maagizo au ni Jeshi la Polisi?” alihoji Lissu, ambaye amewahi kukamatwa mara kadhaa na kulala mahabusu.
Mwanasheria
huyo wa kujitegemea alisema kupinga Serikali si dhambi na haijawahi
kuwa dhambi wala kosa la jinai. Pia, alisema kama unatoa kauli kwa
kuonyesha ubovu au kukosoa, si uchochezi.
Akijua
kuwa alikuwa akitoa kauli kali dhidi ya Serikali, Lissu alisema
anaamini waandishi wa habari hawataandika yote aliyosema kwa sababu
wanaogopa sheria zilizopo, maonyo na vitisho.
0 Comments