Watu
53 wanaosadikiwa kuwa wavuvi wamenusurika kifo baada ya boti yao
kukumbwa na dhoruba na kuzama baharini eneo la Mkokotoni, Mkoa wa
Kaskazini Unguja.
Akizungumzia
tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Hasina Ramadhan Tawfiq
alisema boti hiyo inafahamika kwa jina la Advantage na watu hao
waliokolewa, na baada ya matibabu katika hospitali za Tumbatu na Kivunge
waliruhusiwa kurejea makwao.
Hasina
alisema taarifa za tukio hilo walizipata juzi jioni baada ya kuokolewa
kwa mmoja wao na meli ya Azam Link iliyokuwa ikitokea Pemba kwenda
Unguja na kuwa boti hiyo ilizama saa nne asubuhi. Kamanda huyo alisema
jitihada za uokoaji zilifanywa na vikosi vya KMKM, ZMA na Polisi.
Mvuvi
aliyeokolewa, Khatib Khamis ambaye ni mkazi wa Mtoni alisema chanzo cha
tukio hilo ni upepo mkali ulioambatana na mawimbi yaliyosababisha
chombo chao kupinduka. Alisema kabla ya tukio hilo walikuwa wanatokea
Mtoni kuelekea Kisiwa cha Tumbatu kuvua.
0 Comments